Kocha Mkuu wa Geita Gold FC, Denis Kitambi amesema bado ana imani na kikosi chake licha ya kupoteza mechi tatu mfululizo Ligi Kuu soka Tanzania Bara.

Geita haijaonja ladha ya ushindi katika michezo mitatu mfululizo ikiwa chini ya Kocha Kitambi ambaye alirithi mikoba ya Hemedi Suleimani Morocco.

Kitambi amesema mifumo mipya ya uchezaji na makosa madogo madogo yanayofanywa na wachezaji wake ndiyo yalichangia wapoteze mechi hizo, lakini anafurahi kuona kuna mabadiliko makubwa ya uchezaji kwenye timu yake.

“Ni kweli hatujafanya vizuri kwenye mechi tatu zilizopita, lakini hiyo haiwezi kuwa sababu ya kushuka daraja, bado tuna mechi nyingi za kurekebisha makosa yetu, pia tumebadili mifumo ya uchezaji ambayo wachezaji wangu wameanza kuizoea,” amesema Kitambi.

Vipigo hivyo vitatu vimeiweka Geita FC katika nafasi ya 14 kwenye msimamo wa ligi hiyo ikikusanya Pointi 16 katika idadi kama hiyo ya mechi walizocheza.

Kocha huyo amesema pamoja na kufungwa lakini anajivunia ubora wa kiwango kinachooneshwa na timu yake katika mechi zote, ambazo wamecheza timu ikiwa chini yake.

Freddy Koublan: Ninawafahamu vizuri Asec
Solskjaer afikiriwa FC Bayern Munich