Kiungo wa Mabingwa wa Soka nchini Ujerumani FC Bayern Munich na Ujerumani, Joshua Kimmich, ana hatihati ya kuendelea kusalia kwenye kikosi cha wababe hao kwa kile kinachoelezwa kwamba hana uhusiano mzuri na kocha Thomas Tuchel.
Inadaiwa hivi karibuni Kimmich mwenye umri wa miaka 29, alijibizana na mmoja kati ya wasaidizi wa Tuchel na vilevile mara kadhaa kocha huyo amekuwa hampangi kwenye mechi muhimu za ligi.
Hali hiyo inaripotiwa kumkera staa huyo kiasi cha kutamani kuondoka ili kupata sehemu atakayokuwa na uhakika wa kucheza na kuwa na furaha.
Kimmich amekuwa akihusishwa na timu nyingi kutoka England zikiwamo Manchester United, Liverpool na Arsenal, lakini changamoto ni kwa Bayern ambayo inahitaji mkwanja mrefu.
Mkataba wa Kimmich wa sasa unatarajiwa kumalizika 2025 na msimu huu amecheza mechi 26 za michuano yote, akifunga bao moja na kutoa asisti sita.