Jukwaa la Maprofesa wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania – OUT, limejipanga kuhakikisha linachangia kuinua na kuimarisha shughuli zote za kitaaluma, tafiti na huduma za ushauri wa kitaalamu zinazosimamiwa na chuo hicho, kwa manufaa mapana ya Taifa.
Lengo hilo, limefikiwa kwa pamoja na wajumbe wa jukwaa wakati wa mkutano wake wa tatu ulioanza Februari 15 – 17 katika Kampasi ya Chuo cha Uongozi cha Mwl. Julius Kambarage Nyerere, kilichopo Kibaha Mkoani Pwani.
Akiongea wakati wa kufunga jukwaa hilo, Kiongozi wa jukwaa ambaye pia ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Taaluma, Tafiti na Huduma za ushauri wa kitaalamu Prof. Deus Ngaruko, amesisitiza kuwa jukwaa hilo ni sehemu pekee ambalo wanazuoni wanaweza kukaa na kujadili mambo yao kwa utulivu na kufikia mikakati itakayoleta tija kwa Taasisi na Taifa.
Amesema, “tumejadiliana na kukubaliana mengi lakini kinachotakiwa sasa ni kushirikiana na taasisi, makampuni na wanataaluma wenzetu wote ndani ya chuo na popote ulimwenguni katika kuandika na kusimamia miradi itakayosaidia kuinua na kuboresha maisha ya jamii zetu.”
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo na Mjumbe wa Jukwaa hilo, Prof. Elifas Bisanda amewataka wajumbe hao kuwa Viongozi kitaaluma, ili kuwa mfano bora kwa wasomi wote wanaowaangalia kama dira ya mafanikio.