Aliyewahi kuwa Msemaji wa Klabu za Simba SC na Young Africans Haji Manara amesema Uongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), unapaswa kumfukuza Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, Adel Amrouche kutokana na vitendo vyake viovu ikiwa ni pamoja na kuihujumu Klabu ya Young Africans kuelekea mchezo wao wa Mzunguuko watano wa Kundi D, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya CR Belouizdad.
Young Africans itakuwa mwenyeji wa mchezo huo keshokutwa Jumamosi (Februari 23) katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, huku ikihitaji ushindi ili kufufua matumaini ya kutinga Hatu ya Robo Fainali ya Michuano hiyo.
Kauli hiyo ya Manara imekuja kufuatia Kocha huyo kudaiwa kuwapokea wapinzani wa Young Africans, CR Belouizdad katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere na kuketi nao Serena Hotel jijini Dar es salaam.
Taarifa hizo zimekwenda mbali zaidi zikidai kuwa Kocha Amrouche anadaiwa kuwaibia mbinu CR Belouizdad, ambazo huenda zikawasaidia katika mchezo dhidi ya Young Africans, jambo ambalo limetafsriwa kuwa ni kulihujumu kwa Taifa la Tanzania.
“Pamoja na Ualgeria wake, yeye ni Kocha wa Timu ya Taifa ya Tanzania, kwa nini ashiriki kuihujumu Timu inayotoka ya Tanzania? Sawa klabu inayocheza ni ya Tanzania na inacheza na timu kutoka Algeria, na yeye ni Mualgeria, alipaswa aweke Ualgeria wake pembeni, nadhani TFF wanapaswa kufanya jambo.
“Kumekuwa na tuhuma nyingi sana juu ya huyu kocha, mengine tunayafumba tu kwa sababu ya maslahi ya Timu ya Taifa. Kuna mambo mengi nimeyasikia na mengine kutoka kwa wachezaji wa Taifa Stars aliyoyafanya na anayoendelea kuyafanya kwa timu yetu, tuliacha kwa sababu Stars ilikuwa inashiriki AFCON.
“Lakini hili analolifanya kwa Young Africans na ni timu ambayo inawakilisha nchi ya Tanzania, dhidi ya timu ya nchi yake (CR Belouizdad) wakati yeye ni kocha wa Timu ya Taifa ya Tanzania, analikosea heshima Taifa.
“Pale Serena kuna kamera za CCTV kila mahali, Airport ni kamera za CCTV kila eneo, wafanye uchunguzi, ni kitendo cha dakika moja tu TFF wakaomba ushahidi Serena na Airport watapewa tangu alipoingia mpaka anondoka.
“Na kama itabainika kuwa huyu anayefanya haya ni Kocha wa Taifa Stars, basi TFF wamchukulie hatua, na hatua ya kwanza ni kumfukuza tu. Kocha wa aina hii ni kumfukuza tu wala sio kumfuga. Abaki na Ualgeria wake atuachie Taifa Stars yetu. Kama anasema atachukua hatua na sisi tutatumia wanasheria wetu nini cha kufanya.
“Kocha analetwa hapa analipwa na Serikali lakini anashiriki kuihujumu Young Africans na Taifa, hatuwezi kufuga hawa watu. Kocha mwenyewe haeleweki timu inacheza vipi, pata umpatae, mechi ikichezwa hujui utafungwa saa ngapi, kocha wa nini huyu, aende kwao tu.
“Timu ya Young Africans inayocheza kuna wachezaji wa Timu ya Taifa na pengine kuna wachezaji wengine ambao yeye anatakiwa awatazame ili awaongeze kwenye kikosi chake. Hawa makocha ndio wanaosababisha Timu ya Taifa inapocheza watu wanashindwa kuishabikia kwa sababu ya mambo ya hovyo wanayoyafanya,” amesema Manara.
Ikumbukwe kuwa, Amrocuhe amesimamisha na TFF kuinoa Taifa Stars baada ya kutoa kauli za kichochezi kati ya Tanzania dhidi ya Taifa la Morocco wakati wa ‘AFCON 2023’ akidai kuwa CAF imekuwa ikilipendelea taifa hilo la Afrika Kaskazini.