Historia ya Mwamuzi wa kati Boubou Traore (34) kutoka Mali, inazilazimisha Young Africans na Belouizdad kila moja kujipanga vilivyo wakati zitakapokutana katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam, keshokutwa Jumamosi (Februari 24) kuanzia saa 1:00 usiku.

Traore ndiye amepangwa na Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’, kushika kipenga katika mechi hiyo ya Ligi ya Mabingwa Afrika akisaidiwa na Sydou Tiama (Burkina Fasso), Nodibo Samake (Mali) na mwamuzi wa mezani Ousmane Diakate kutoka Mali.

Mwamuzi huyo ameonekana kuwa na historia ya bahati kwa timu za kutoka ukanda wa nchi zinazozungumza lugha ya Kiarabu lakini pia amekuwa na kumbukumbu mbaya kwa CR Belouizdad katika mechi ambazo huwa wanchezeshwa naye.

Katika mechi 10 zilizopita ambazo timu za Kiarabu zilicheza huku Mwamuzi akiwa Traore, ziliibuka na ushindi mara tisa na moja ikitoka sare.

Lakini pamoja timu nyingi kutoka Uarabuni kuwa na historia ya kufanya vyema pindi zinapochezeshwa na Traore, Mwamuzi huyo amekuwa na nuksi kwa Belouizdad kwani haijawahi kupata ushindi au hata sare pale alipoichezesha.

Traore amechezesha mechi mbili za Belouizadad ambapo ya kwanza ni ile iliyocheza Februari 28, 2021 dhidi ya Mamelodi Sundowns Uwanja wa Benjamin Mkapa ambayo timu hiyo kutoka Algeria ilichapwa mabao 5-1.

Februari 24, 2023, CR Belouizdad ilipoteza kwa bao 1-0 mbele ya Al Merrikh huku Mwamuzi wa mchezo akiwa ni Boubou Traore.

Young Africans inayoshika nafasi ya tatu kwenye Kundi D la Ligi ya Mabingwa Afrika, inahitaji ushindi katika mechi hiyo dhidi ya Belouizdad ili ifkishe alama nane na kuweka hai matumaini yake ya kuingia hatua ya Robo Fainali.

Kwa sasa, msimamo wa kundi hilo unaongozwa na Al Ahly ya Misri yenye alama sita, ikifuatiwa na Belouizdad kisha Young Africans ambazo zina alama tano kila moja na Medeama iko mkiani na alama zake nne.

Kitambi: Ratiba inatuumiza sana
Twiga Stars kazi wanayo