Chama cha Waajiri Tanzania – ATE, kimeipongeza Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) kwa kuwa mstari wa mbele katika kutoa nafasi za juu za uongozi kwa wanawake ikiwa ni pamoja na kuwapitisha kwenye mafunzo maalum ya Uongozi – Female Future Tanzania (FFT) yanayoratibiwa na kuendeshwa na chama hicho.
Hayo yamebainishwa mwishoni mwa wiki Mjini Geita na Mkuu wa Idara ya Mafunzo na Ujuzi, Albert Rukeisa kwa niaba ya Ofisa Mtendaji Mkuu wa ATE, Suzanne Ndomba – Doran ambapo pamoja na mambo mengine amesema GGML imefanikiwa kufundisha wanawake 23 katika ngazi ya juu ya uogozi.
Alisema, idadi hiyo ya wafanyakazi wanawake wa GGML waliopatiwa mafunzi ni sawa na asilimia sita ya washiriki kutoka mashirika binafsi na kwamba GGML imeendelea kuchangia katika kuendeleza ujuzi katika taifa kupitia program mbalimbali ikiwamo ya mafunzo tarajali kwa wahitimu wa vyuo vikuu wasiokuwa na ajira.
“Jitihada hizi zenye zaidi ya miaka 15 zimekuwa chachu kwa waajiri wengine kuendelea kutoa nafasi kwa vijana kujifunza na kuongeza wataalam wa madini katika sekta hii,” aliongeza.
“GGML ni miogoni mwa waajiri bora hapa Tanzania na umeshinda mara kadhaa kwenye tuzo za mwajiri bora wa mwaka zinazoandaliwa na kuratibiwa na chama cha waajiri Tanzania.
“Sanjari kutambuliwa na waajiri, mgodi huu umekuwa na mahusiano mazuri na ushikishwaji madhubuti kwa chama cha wafanyakazi katika kuendesha mgodi,” alisema Rukeisa.
Aidha, alitoa mfano kuwa mwaka jana, Mgodi huo uliingia mkataba wa hali bora na chama cha wafanyakazi hivyo ATE wanajivunia kuwa sehemu ya mafanikio hayo.
Alisema mbali na program hizo za kuwapatia mafunzo kwa vitendo wahitimu hao wa vyuo vikuu, pia GGML imekuwa mstari wa mbele katika suala la jinsi na jinsia.
Kwa mujibu Makamu Rais Mwandamizi – Kitengo cha masuala ya Ubia/ushirika Afrika kutoka AngloGold Ashanti – GGML, Terry Strong, mojawapo ya vipaumbele vya kampuni hiyo ni kuendelea kuboresha usawa wa kijinsia katika majukumu yao ya kibiashara ili kuiwakilisha jamii husika sehemu wanapofanyia kazi.
Terry alisema kampuni hiyo imeendelea kufanya kazi kubwa kuhakikisha malengo ya kuwawezesha wanawake kujiunga na sekta hii ya madini yanafanikiwa.
Mmoja wa wanufaika wa program za kuwapatia mafunzo kazini wahitimu wa vyuo vikuu ni Evelyine Julius ambaye alihitimu mafunzo hayo mwaka jana kisha kupatiwa ajira ya kudumu kupitia program African Business Unit (ABU).
Evelyine ambaye ni mhandisi wa masuala ya umeme alisema “nimejifunza vitu vingi ikiwamo namna kazi zinavyofanyika kwa vitendo. Uwepo wangu GGML ni fursa ya kipekee kwa sababu nitaweza kutekeleza miradi mbalimbali kwa ujasiri na ujuzi nilioupata,” alisema.
Mkunde Frank ambaye ni mteknolojia wa masuala ya jiolojia, naye alisema nafasi aliyoipata ya kuendelea kufanya kazi ndani ya GGML kupitia progamu ya ABU, imeendelea kumjengea kujiamini na kunoa zaidi ujuzi wake.
“Mathalani kwenye kitengo cha geolojia tumepata fursa ya kipekee, kila mfanyakazi anapewa uthamani bila kujali mkubwa au mdogo. Lakini hata ukishuka kwenye machimbo chini ya ardhi kila mfanyakazi anazingatia mafunzo aliyopewa kwa vitendo hasa katika kutekeleza kipaumbele cha kwanza ambacho ni usalama,” alisema.