Bodi ya Ligi Kuu Tanzania ‘TPLB’, imezipongeza timu za Simba SC na Young Africans kwa kufanya vizuri katika michezo yao ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwishoni mwa juma lililopita.

Afisa Mtendaji Mkuu wa TPLB, Almas Kasongo, amesema, Simba SC imefanya kazi kubwa kupata alama moja muhimu ikiwa ugenini dhidi ya Asec Mimosas ya Ivory Coast, wakati Young Africans ikifanikiwa kufuzu hatua ya Robo Fainali baada ya ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya CR Belouizdad ya Algeria kwenye iliyopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa.

“Ninazipongeza Simba SC na Young Africans kwa kufanya vizuri katika michezo yao ya kimataifa. Young Africans imeonyesha uwezo mkubwa na kuweza kuingia hatua ya Robo Fainali kwa kuifunga timu ya CR Beloufzdad kwa idadi kubwa ya mabao, lakini Simba SC pia ilipata alama moja muhimu ugenini, naamini mchezo wa nyumbani itafanikiwa na kusonga mbele,” amesema Kasongo.

Mtendaji huyo wa TPLB, amesema kutokana na ubora wa timu ya Simba SC, anaamini itapata matokeo mazuri itakapoikaribisha Jwaneng Galaxy, kwani Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, anafanya juhudi kubwa kuhakikisha michezo inazidi kukua.

“Ni wakati wa Watanzania kuungana pamoja na kujitokeza kwa wingi ifikapo tarehe mbili (mwezi ujao) kwa ajili ya kuisapoti timu yetu, kufanikiwa kwa Simba SC ni furaha ya Taifa kwa ujumla,” amesema Mtendaji huyo

Aidha, ameongeza kuwa Shirikisho la Soka Tanzania ‘TFF’, kwa kushirikiana na TPLB wamepanga mikakati ya muda mrefu kuhakikisha timu zinafanya vizuri nje na ndani ya nchi.

“Ni mipango yetu ya muda mrefu ambayo tumejiwekea kuhakikisha timu zetu zinafanya vema kwenye mashindano ya Kimataifa nje na ndani ya nchi, mafanikio tumeanza kuyaona,” amesema

Tshabalala: Kazi tutaimaliza nyumbani
Baada ya miaka 58: Magubike wapata Gari la kubebea Wagonjwa