Rais wa Klabu ya Young Africans, Hersi Saidi amesema mikakati yao kuelekea mechi ya Robo Fainali ni kuongeza hamasa kwa Wachezaji na Benchi lao la Ufundi kuzidi kufanya vizuri kwenye hatua hiyo.

Young Africans Jumamosi (Februari 24) ilikata tiketi ya kucheza Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya CR Belouizdad ya Algeria.

Kitendo cha Young Africans kutinga hatua hiyo kitaifanya kupokea kitita cha Dola za Marekani 900,000 ambazo ni sawa na Sh bilioni 2.4.

Kiasi hicho cha fedha ukijumuisha na hamasa kutoka kwenye uongozi wa timu hiyo chini ya Rais Hersi, kunawapa wachezaji wa Young Africans morali kubwa na huenda ´wakaoga noti kufuatia mafanikio wanayoyapata katika michuano hiyo.

Lengo letu ni kuwaongezea ari ya upambanaji wachezaji wetu. Awali lengo letu lilikuwa kufika makundi na wamefanya hivyo na katika hatua hii, baada ya kuwajua wapinzani wetu tukasema tucheze na tutakubali matokeo yoyote, nafurahi kuona tumetinga Robo Fainali.

“Sasa baada ya kufika Robo Fainali, lengo letu ni kuongeza hamasa kwa wachezaji wetu na benchi la ufundi ili tuweze kushinda na hilo likitokea tutaongeza bonasi nyingine zaidi ya ilivyokuwa hatua zilizopita, na ikishindikana hatuwezi kuwadai sababu hapa tulipofika tumevuka malengo tuliyokuwa tumejiwekea,” amesema.

Wakati Rais wa klabu hiyo akitoa ahadi nono, Kocha Mkuu Miguel Gamondi amesema, kiu yake ni kuiona Young Africans inafika mbali zaidi ya hapo na anaamini hilo linawezekana kutokana na ubora wa kikosi chake, lakini pia ugumu waliokutana nao kwenye mechi za makundi.

“Tuna kikosi bora sana ambacho kama tukiongeza umakini tunaweza kufanya makubwa zaidi ya haya, ingawa baadhi ya watu walitubeza baada ya kupoteza mchezo wa kwanza dhidi ya Belouizdad kwao, najivunia sana ubora wa wachezaji wangu sababu na sapoti ya mashabiki, miaka 25 kukaa bila kufika hapa si jambo, dogo,” amesema Gamondi.

Ancelotti: Sitaingilia maamuzi yake
Twiga Stars kurusha karata muhimu