Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amesema kuwa kazi ya uchorongaji wa visima vya Jotoardhi nchini Tanzania itaanza mwezi Aprili mwaka huu ili kuweza kuhakiki rasilimali ya Jotoardhi iliyopo kabla ya kuanza kwa shughuli za uzalishaji umeme kutokana na nishati hiyo.

Dkt. Biteko amesema baada ya kutembelea vyanzo na mitambo ya kuzalisha umeme wa Jotoardhi katika Mji wa Naivasha, Kaunti ya Nakuru nchini Kenya.

Amesema, “tumekuja kwenye mitambo ya kuzalisha umeme unaotokana na Jotoardhi inayomilikiwa na kampuni ya uzalishaji umeme ya Kenya (KenGen) na tumejionea jinsi walivyopiga hatua kwenye uendelezaji wa rasilimali hii kwani tayari wanazalisha umeme wa Jotoardhi wa kiasi cha megawati zaidi ya 799.”

Aidha, amesema tayari Tanzania imetenga fedha kwa ajili ya kuendeleza vyanzo vya Jotoardhi na kwamba kampuni ya KenGen mwezi Aprili mwaka huu itakuwa mkoani Mbeya kwa ajili ya kuanza uchorongaji vyanzo vya Jotoardhi katika eneo la Ngozi na Kiejo-Mbaka kwa kushirikiana na kampuni ya Uendelezaji wa Jotoardhi Tanzania (TGDC).

Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa Maendeleo ya Jotoardhi katika kampuni ya KenGen, Peketsa Mangi amesema kuwa, nchi hiyo imekuwa na ushirikiano mzuri na Tanzania katika kuhakikisha nchi hizo zinafanikiwa katika uendelezaji wa Jotoardhi.

 

Viongozi walioambatana na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati kwenye ziara hiyo ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Stephen Byabato, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Benard Kibesse na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga.

 

RC Telack: Lindi, Kilwa jiandaeni kuwapokea Watalii
Tuzo umahiri wa Uandishi Habari za Wanawake na Uongozi zimewadia