Kiungo Mshambuliaji wa Young Africans Stephane Aziz Kl, amesema moto alioanza nao Joseph Guede bado kabisa, kwani anamjua ni mchezaji hatari linapokuja suala ya kucheka na nyavu, sema alikuwa akijitafuta tangu atue Jangwani.

Aziz KI amesema Guede aliyefunga mabao matatu katika mechi mbili zilizopita, mawili katika Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ na lile muhimu zaidi lililoipeleka Young Africans hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, ni mchezaji hatari na wale waliokuwa wakimchukulia poa, basi wajiandae kupata aibu wakati huu gari lake likiwa limeshaanza kuwaka.

Guede alifunga bao la nne wakati Yanga ikiizamisha CR Belouizdad kwa mabao 4-0, pasi yake ikitokea kwa Aziz KI ambaye amesema anamfahamu nyota huyo na kwamba moto wake bado haujawaka kisawasawa ila utawachoma wengi.

Aziz amesema mabao ambayo ameanza kufunga Guede ni mwanzo tu, kwani anamfahamu vilivyo uimara wake kwenye eneo la kucheka na nyvu.

Amesema uwezo atakaouonyesha utaendelea kuwashangaza kwani anamtambua mshambuliaii huyo vizuri.

“Wakati akiwa FAR Rabat alikuwa akija Ivory Coast kwa ajili mapumziko na walikuwa wakifanya mazoezi na niliwahi pia kumfuatilia kwa ufupi.

“Sina wasiwasi, atafunga sana ila alihitaji muda wa kuzoea mazingira na namna ya uchezaji lakini pia watu wasisahau kuwa alikuwa nje kwa kipindi kidogo.”

“Mchezaji yeyote uwezo wake upo katika kucheza mechi kubwa zenye ushindani ndio maana alipokuja alikuwa na wakati mgumu wa kujitafuta kwanza, ila kwa nafasi hizi anazopewa sasa mashabiki watamsahau,” amesema Aziz.

Nyota huyo Mghana ni miongoni mwa wachezaji 24 waliopo Cairo, Misri na kikosi cha Young Africans kitakachokabiliwa na mchezo wa hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Al Ahly utakaopigwa leo Ijumaa (Machi Mosi) saa l:00 usiku, kila timu ikisaka heshima ya kumaliza kinara wa Kundi D, huku zote zikifuzu hatua ya Robo Fainali.

Muhimbili kuandaa mpango wa dharura huduma NHIF
Kimiti ahimiza uwajibikaji Shirika la Nyumbu Kibaha