Kocha Mkuu wa Mtibwa Sugar, Zuberi Katwila, amesema kazi aliyonayo kwa sasa ni kuwatengeneza kisaikolojia washambuliaji wake ili wawe watulivu wanapokuwa langoni kwani wanapoteza nafasi nyingi za kufunga.
Katwila amesema timu yake ingeweza kuibuka na ushindi katika mchezo huo, lakini washambuliaji wake walikuwa wakibabaika na kushindwa kuwa na utulivu kila walipokuwa kwenye nafasi ya kuuweka mpira wavuni.
“Najua hii yote ni kwa sababu hatushindi mechi zetu, tunapitia kwenye wakati mgumu kiasi kwamba wachezaji wanapokuwa kwenye nafasi ya kufunga wanatetemeka na kupoteza nafasi, hili ni suala siyo tena la kiufundi ila ni la kisaikolojia,”
“Itabidi nikae nao nione jinsi gani ya kuwasaidia, huku kwenye ufundi tumejitahidi sana, timu inacheza vizuri, wachezaji wangu walipambana, walitumia ufundi, nguvu, na kila kitu, lakini wenzetu waliweza kutuzuia vizuri, ndiyo mpira, hatupo kwenye wakati mzuri, inabidi kuendelee kupambana,” amesema Katwila.
John Baraza, Kocha Mkuu wa Dodoma Jiji kwa upande wake ameshangaa kwa jinsi Mtibwa walivyocheza katika mechi hiyo tofauti na jinsi alivyoizoea na kuisoma.
“Tulijua watakuja kucheza kama tulivyodhani, haikuwa hivyo, walitushambulia kwa nguvu kiasi kwamba ikabidi niweke mabeki watano nyuma badala ya wanne, nawapongeza vijana wangu, alama moja mimi kwangu ugenini siyo mbaya,” amesema Baraza.
Matokeo ya mechi hiyo, yanaifanya Mtibwa kuendelea kuburuza mkia ikiwa na alama tisa, Dodoma Jiji ikishika nafasi ya 10, ikiwa na alama 20.