Hatma ya Mshambuliaji Mason Greenwood kwenye kikosi cha Manchester United itafahamika nwishoni mwa mwezi Mei mwaka huu, imeelezwa.
Mmiliki mpya wa miamba hiyo ya Old Trafford, bilionea Sir Jim Ratcliffe amewataka watu wanahusika na masuala ya kuhusu mshambuliaji huyo anayecheza kwa mkopo Getafe kwa sasa, kuhakikisha wanapata ufumbuzi wa jambo lake kati ya sasa hadi mwisho wa msimu.
Bosi huyo anataka kuzungumza na makundi ya mashabiki pamoja na maofisa wengine wakubwa kwenye klabu hiyo juu ya suala la Greenwood kabla ya kufikia uamuzi wa mwisho.
Kinachoelezwa ni kwamba Kocha Erik ten Hag amefungua milango ya kumkaribisha kikosi staa huyo, lakini kama tu jambo hilo litaungwa mkono katika kila idara.
Chanzo cha karibu kilifichua: “Jim Ratcliffe anataka jambo hilo limalizwe hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Mei, ili ikifika kipindi cha usajili cha majira ya joto kila kitu kiwe kimefahamika.
“Kuna timu zinamtaka Mason wakiwamo Barcelona, lakini uhamisho huo hauwezi kuzunguzwa kwa sasa hadi hapo itakapofahamika mwishoni mwa Mei. Kwa sasa hivi, mambo yapo nusu nusu kuhusu Mason kurudi.”
Tajiri Ratcliffe imeelezwa kwamba yupo tayari kuwarudisha kwenye kikosi Greenwood pamoja na Jadon Sancho. Mara ya mwisho Greenwood kuichezea Man United, ilikuwa Januari 2022.
Sancho naye kwa sasa yupo kwa mkopo Borussia Dortmund baada ya kutibuana na kocha Ten Hag.
Tajiri Ratclife alisema: Tutafanya uamuzi. Sifahamu kama Greenwood bado atahitaji kuwa nasi. Yeye ni mchezaji wa Man United na sisi tunawajibika na mambo ya soka. Tutafanya uamuzi.”