Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans, Miguel Angel Gamondi, amesema mechi nne zilizopo mbele yake zinatosha kuwa mazoezi ya kujiandaa na mechi ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Jumanne ijayo (Machi 12) Young Africans inatarajia kujua mpinzani wake wa hatua ya Robo Fainali Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, wakati Droo hiyo itakapochezeshwa nchini Misri majira ya saa tisa alasiri kwa saa za Afrika Mashariki.
Katika Droo hiyo, Young Africans inaweza kukutana na Petro de Luanda ya Angola, Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini ama Asec Mimosas ya Ivory Coast huku watani zao Simba wenyewe wanaweza kukutana na Al Ahly ya Misri, Mamelodi Sundowns ama Petro de Luanda.
Kocha huyo ambaye timu yake inajiandaa kucheza dhidi ya Namungo FC kesho Ijumaa (Machi 08), Uwanja wa Majaliwa mkoani Lindi, amesema michezo minne iliyopo mbele yake itakuwa ni ya kuwaandaa wachezaji wake wawe fiti kwenye mechi hiyo ya kimataifa.
“Tumerejea kwenye mechi za ligi ambazo tutazitumia kutafuta ushindi, lakini hizi hizi tutatumia kujiandaa na mechi za Robo Fainali, zitatufanya tuwe imara, na Machi 12 Droo itakapopangwa tutaongeza kitu kingine, nacho ni kujua mpinzani gani tutacheza naye na kuanza mazoezi maalum kwa ajili ya kumkabili kutokana na mbinu zao tutakazozisoma,” amesema Gamondi.
Amekiri kuwa michezo ya kimataifa huwa ni migumu na yenye mbinu zaidi, lakini atafanya kila njia kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa kwa wachezaji wake.
“Mechi za makundi zilikuwa ngumu na ushindani mkubwa, lakini vijana wamepambana kwa kila hatua na kufanikiwa kufika hatua ya Robo Fainali kwa kuvuka malengo yetu,” amesema
Gamondi amewataka wachezaii wake wacheze mechi za Ligi Kuu kama ambavyo walikuwa wakicheza kwenye Ligi ya Mabingwa na wasiidharau timu yoyote kwani ushindi wa ligi ndiyo unaowapeleka kucheza mechi hizo kubwa.
“Kuna tabia ya baadhi ya wachezaji wakishapata ushindi kwenye mechi hizi kubwa morali yao inashuka na hawajitumi kwenye michezo ambayo wao wanaona ni midogo, hii si sawa, sehemu hii ndiyo timu inapata uwakilishi, tunahitaji pointi kila mchezo kupata nafasi ya kurudi tena mwakani, pia kuwapa furaha mashabiki wetu,” amesema Gamondi.
Baada ya mechi hiyo, Young Africans itakuwa nyumbani, Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es salaam kucheza dhidi ya Ihefu, Machi 11, siku tatu baadae, Machi 14, itashuka tena Uwanjani hapo kucheza dhidi ya Geita Gold na siku zingine tatu baada ya hapo, Machi 17, itacheza kwenye Uwanja huo dhidi ya Azam FC.
Hata hivyo, katika mechi hiyo, Young Africans itakuwa mgeni kikanuni na baada ya hapo, itapata mapumziko ili kujiandaa na mechi ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika inayotarajiwa kupigwa kati ya Machi 29 mpaka 31.