Kocha Mkuu wa Azam FC Youssoupha Dabo amesema hakutakuwa na wala hakuna pengo la Mshambuliaji kutoka nchini Zimbabwe Prince Dube, ambaye ni dhahir ataondoka klabuni hapo.

Dube aliyeifungua Azam mabao saba msimu huu na kutoa pasi mbili za mabao ameshaaga klabuni na yupo kwenye harakati za kuvunja mkataba ili msimu ujao awe mchezaji huru, japo mabosi wa klabu hiyo wamemkomalia wakisema wana mkataba naye na kuuvunja lazima alipe zaidi ya Sh700 milioni.

Taarifa zinasema kuwa mshambuliaji huyo alianza kwa kugomea kila programu aliyokuwa akipewa mazoezini na makocha wake, jambo lililoanza kumvuruga Dabo.

Kocha huyo raia wa Senegal amesema haoni pengo la mshambuliaji huyo kwenye timu kwa kuwa ana wachezaji wengine ambao wanaweza kufanya kazi anazowatuma.

“Tumemkosa kwenye mechi mbili dhidi ya Tanzania Prisons tukamaliza mchezo kwa sare ya bao 1-1, tumeshinda mabao 4-1 dhidi ya Dodoma Jiji na sare ya bao 1-1 dhidi ya Coastal Union. Wachezaji waliopo wameweza kufanya vizuri,” amesema kocha huyo.

“Azam ina wachezaji wengi na kila mmoja anatamani kupata nafasi ya kucheza, hivyo naamini waliopo watafanya vizuri eneo hilo bila kujali Dube yupo au hayupo.”

Dube alisajiliwa na Azam mwaka 2020, kutoka Highlanders ya Zimbabwe na kumaliza msimu wa kwanza akiwa na mabao 14, akicheza katika mechi 11 kabla ya kupata majeraha na msimu uliopita alirudi kwa kasi akifunga mabao 11. Hivi karibuni ameanzisha mgomo baridi akiwa na mabao saba katika mechi tisa za ligi.

Dube ambaye alikuwa mshambuliaji kiongozi katika kikosi cha Azam (namba tisa) mwishoni mwa juma lililopita aliripotiwa kuanza mchakato wa kuondoka nchini kwenda kwao Zimbabwe.

Azam FC katika michezo 20 imefanikiwa kushinda 13, sare michezo mitano na kupoteza mitatu, huku washambuliaji wake wakifunga mabao 45 na kuruhusu 15 wakiwa na pointi 44.

Mohamed Salah afichua kuondoka Liverpool
Mawaziri SADC watuma salamu za rambirambi JMT