Mtendaji Mkuu wa zamani wa Bayern Leverkusen, Reiner Calmund amemshauri Kocha wa miamba hiyo ya Bundesliga Xabi Alonso kuwa mvumilivu hadi atakaposikia Kocha wa Real Madrid, Carlo Ancelotti ameondoka ili akachukue nafasi yake.
Alonso amekuwa akiwindwa na miamba ya soka Barani Ulaya zikiwemo Bayern Munich, Liverpool na FC Barcelona lakini baada ya kushtukia hilo, mtendaji huyo anaamini Madrid ndio sehemu sahihi zaidi kwa kocha huyo anayefanya vizuri Leverkusen na ikishindikana bora aendelee kusalia hapo kuliko kwenda Liverpool ama Bayern Munich.
“Sidhani kama Alonso atajiunga na Liverpool, ingawa ni kweli ni timu nzuri, amewahi kushinda Ligi ya Mabingwa akiwa hapo (Liverpool), na kushinda mataji matatu ya Ligi Kuu Ujerumani akiwa na Bayern, hakuna ubishi ni sehemu nzuri lakini tunatakiwa kwanza tuone nini kitatokea pale Madrid,”
“Ikiwa Ancelotti hatoondoka kwa sasa, mimi ningekuwa wakala wake nisingemshauri aende Liverpool, ningemwambia asubiri kwa mwaka mmoja au miwili ili aende Madrid,” alisema na kuongeza kuna asilimia nyingi Alonso akaendelea kuifundisha Leverkusen kwa msimu ujao.
“Kuna habari nyingi zinasemwa na kuandikwa, hautakiwi kuamini, sihitaji kuwa mtu anayetabiri ndoto lakini naweza kukwambia nina uhakika wa asilimia kadhaa Alonso ataendelea kuwa Leverkusen kwa msimu ujao.”
Moja ya sababu ambazo zinamfanya Calmund aamini Alonso hatakiwi kutua Liverpool kama mbadala wa Klopp kwa sasa ni presha kubwa ambayo ipo kwenye kikosi hicho.
Klopp ameacha alama kwenye kikosi cha Liverpool na kocha anayekwenda kuchukua mikoba yake, mashabiki watahitaji kuona akiendeleza kwa kasi ile ile.