Meneja Habari na Mawasilino wa Simba SC Ahmed Ally amesema kuna kila sababu ya kikosi chao kupambana kwa nguvu zote, ili kufikia lengo la kucheza Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika kwa mara ya kwanza.
Ahmed Ally ametoa kauli hiyo kufuatia Simba SC kupangwa kukutana na Mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika Al Ahly, katika mchezo wa Robo Fainali.
Kiongozi huyo amesema dhamira kubwa ya Simba SC msimu huu ni kucheza Nusu Fainali ya michuano hiyo, baada ya kuishia Robo Fainali katika michuano ya kimataifa kwa miaka minne mfululizo.
“Safari hii tutavunja mwiko kwa kuenda Nusu Fainali, watu wanasema Al Ahly huwa wanabadilika kulingana na hatua husika, Simba SC tunaiona Nusu Fainali licha ya ugumu wa mechi”
“Hatutakubali kurudia makosa tulioyafanya nyuma, mara zote tumekuwa tunashindwa kuitumia michezo ya hapa nyumbani ili kujiweka katika mazingira ya kusomba mbele, safari hii tutahakikisha tunapambana na kushinda nyumbani kwa idadi kubwa ya mabao ili tukienda ugenini tukapambane zaidi na kufikia malengo yetu.” Amesema Ahmed Ally
Simba SC itaanzia nyumbani Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam kuikabili Al Ahly kwenye mchezo wa Mkondo wa Kwanza utakaopigwa kati ya Machi 29 au 30, huku mchezo wa Mkondo wa Pili ukipangwa kupigwa kati ya April 5-6 mjini Cairo, Misri.