Mara nyingi Madereva huwa wanashawishika kulipita gari jingine mara aonapo gari ya mbele yake imetoka na kuanza kulipita gari la mbele yake, hivyo naye kufuata mkondo na kuwa nyuma yake kwa kutembelea hesabu za Dereva husika, tabia ambayo haifai na Hatarishi.
Ukurasa wa Mabalozi wa Usalama Barabarani – RSA, umetoa elimu juu ya hili na kueleza kuwa ajali nyingi zimetokea kwa gari ya nyuma ya ile iliyotangulia kuovateki huku ikisisitiza kuwa magari yote ambayo hutakiwi kuyafuta kwa nyuma, Basi kubwa la abiria ni moja wapo.
RSA wanasema, “chonde chonde usiunge nyuma ya basi, kwani basi linaweza kutoka na kurudi haraka kuliko wewe. wakati basi likiwa mbele yako linaovateki, wewe uoni wako wa gari inayokuja mbele unakuwa hafifu.”
Wanazidi kufafanua kuwa, “iwapo kunatokea gari yoyote mbele ikija kwa spidi, basi likirudi kushoto wewe ndio unatazamana na hilo gari linalokuja uso kwa uso.”
Aidha, RSA wanaarifu kuwa, ajali iliyotokea Kijiji cha Kiromo Bagamoyo, Pwani Machi 10, 2024, chanzo chake ni lori kufuata basi bila kujua nini kinakuja mbele. Matokeo yake ni ajali iliyogharimu maisha ya watu tisa hapo hapo wakiwemo madereva wa Magari yote mawili.
Ajali hiyo, ilihusisha Lori aina ya Howo lenye namba za usajili T 503 DRP likivuta tela lenye namba za usajili T 733 DUQ, lililokuwa likitokea Bagamoyo Pwani kuelekea Dar es Salaam, kugongana na Toyota Coaster yenye namba usajili T 676 DSM, lililokuwa likitokea Dar es Salaam kuelekea Bagamoyo.