Waziri wa Madini wa Jamhuri ya Zimbabwe, Soda Zhemu amesema kuwa Nchi yake imevutiwa na Mifumo ya Minada ya Madini ya Vito iliyo katika hatua za mwisho kurejeshwa nchini Tanzania baada ya kukamilika kwa Marekebisho ya Sheria.
Zhemu aliyasema hayo Machi 12, 2024 mjini Victoria Falls, nchini Zimbabwe katika kikao kifupi na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini Msafiri Mbibo anayeongoza Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa Tisa wa Wataalam na Baraza la Mawaziri wa ADPA unaoendelea mjini hapa.
Awali, Naibu Katibu Mkuu Mbibo alimweleza Waziri Zhemu kuwa, Tanzania iko katika hatua za mwisho kukamilisha Marekebisho ya Sheria itakayoruhusu kurejeshwa kwa Minada ya Vito ambapo alisema kuwa kutakuwa na minada ya aina mbili, mmoja ni wa ndani ya nchi na mwingine ukiwa ni wa Kimataifa.
Mbibo aliongeza kuwa, uwepo wa minada ya ndani ya nchi inatoa fursa kwa wenyeji kushiriki katika soko la madini ya vito kwa kuongeza thamani pamoja na kununua kwa matumizi yao pamoja na biashara.
Kufuatia maelezo hayo ya Mbibo, Waziri wa Madini wa Jamhuri ya Zimbabwe, Mhe. Soda Zhemu alikiri kuvutiwa na muundo wa minada ya madini ya vito iliyo kwenye hatua za mwisho kurejeshwa mara baada ya kukamilika Marekebisho ya Sheria kwa kusema kuwa ni wazo Nchi hiyo italichukua na kulifanyia kazi.
Ameeleza kuwa muundo wa minada iliyopo Zimbabwe haitoi nafasi kwa wenyeji kushiriki bali wageni wamekuwa na nafasi kubwa zaidi ya kuongeza thamani na kununua madini hayo ya vito.
Waziri Zhemu aliongeza kuwa Zimbabwe itaendelea kushirikiana na Tanzania katika Sekta ya Madini ikiwa ni pamoja na kujifunza namna bora ya usimamizi katika Sekta ya Madini ambayo Tanzania imepiga hatua zaidi na kuchukiliwa kama mfano na nchi nyingi barani Afrika.
Kikao hicho kifupi, pia kilihudhuriwa na Katibu Mkuu Wizara ya Madini – Zimbabwe, Pfungwa Kunaka, pamoja na Kamishna Msaidizi wa Madini – Sehemu ya Uendelezaji Uchimbaji Mdogo na Mratibu wa ADPA Tanzania, Francis Mihayo.