Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imefanya ziara Mkoani Arusha kukagua mradi wa ujenzi wa njia kuu ya umeme wenye msongo wa kilovoti 400 katika eneo la Lemugur mkoani Arusha tarehe 13 Machi, 2024.
Wakiongozwa na mwenyeji wao Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga wajumbe wa Kamati hiyo walifanikiwa kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho kitakachounganisha Tanzania na nchi za Afrika mashariki pamoja na Kusini mwa Afrika katika ushirikiano kwenye sekta ya nishati ya umeme.
Akizungumza katika ziara hiyo, Kapinga aliwashukuru wajumbe wa Kamati hiyo kwa kufanya ziara na kutoa ushauri na maelekezo muhimu yanayolenga kufanikisha utekezaji wa mradi huo utakaokuwa mkombozi wa upatikanaji wa umeme katika mkoa wa Arusha na nchi zipatazo 13 na kudai kuwa Serikali imewekeza fedha nyingi katika ujenzi wa kituo hicho takribani dola milioni 258.
Aidha, Kapinga alisema baada ya kukamilika kwa mradi huu tutakuwa na uhakika wa umeme nchini kwa kuwa miundombinu hii itawezesha kusafirisha umeme nje ya nchi na pia kuleta umeme kutoka katika nchi hizo pale tunapokuwa na uhaba wa nishati hiyo ambapo mradi huo unaotekelezwa kwa gharama ya dola za Marekani 258.82 utekelezaji wake umekamilika kwa asilimia 99.6.
Amesema, amepokea ushauri na maelekezo yote ya Kamati hiyo na kuahidi kuyafanyia kazi kwa kuanzia na eneo la usimamizi wa miradi ya umeme ili iweze kumaliza changamoto ya upatikanaji wa nishati ya umeme hapa nchini.
Akitoa maelekezo ya Kamati, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mathayo David Mathayo amelekeza wizara kuhakikisha inasimamia wakandari wote wanaotekeleza miradi ya umeme nchini ili wakamilishe miradi hiyo kwa wakati na kuiwezesha Serikali kupeleka huduma ya umeme kwa wananchi wote kama ilivyokusudiwa.
“Kumekuwa na miradi ya umeme ambayo utekelezaji wake unasuasua kutokana na uzembe unaofanywa na baadhi ya wakandarasi wasio waaminifu waliopewa kazi hizo hivyo Wizara ikahakikishe inawachukulia hatua ikiwemo kuwafungia leseni zao ili wasiwe na sifa za kupata kazi katika nchi yetu,” alisema.