Baada ya kuwafahamu wapinzani wao katika Michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika Hatua ya Robo Fainali, Kocha wa Mamelodi Sundowns, Rhulani Mokwena amesema anakwenda kujichimbia kuitazama zaidi Young Africans kiufundi wakati wa mapumziko ya kalenda ya mechi za kimataifa.

Hivi karibuni timu za mataifa mbalimbali zitakuwa na michezo ya kirafiki na mashindano ya kimataifa, kipindi ambacho ligi zote duniani husimama kupisha mechi hizo.

Mokwena amesema mara kadhaa amekuwa akizitazama mechi za timu zote ambazo zilikuwa na uwezekano wa kukutana nazo, lakini anataka kurudia tena ili kuwatazama kwa umakini zaidi Young Africans.

Kocha huyu amesema anaiheshimu timu hiyo kwa sababu ina muunganiko na uongozi mzuri na kocha Miguel Gamondi ni mmoja kati ya makocha bora na ameshawahi kuwafundisha mabingwa hao mara sita mfululizo wa Ligi Kuu ya Afrika Kusini.

“Nitarudia tena kuwatazama kwa umakini zaidi. Niliwahi kutazama mechi zao, lakini sikuwa nimejikita kwenye kuzichambua zaidi, hivyo nitakwenda kuwatazama tena na jambo zuri nitakuwa na muda mwingi kwa sababu tunakwenda kwenye mapumziko ya kalenda ya kimataifa ya FIFA,” amesema.

Mokwena amesema hayo wakati anafanya mahojiano na waandishi wa habari baada ya mchezo wa Ligi Kuu Afrika Kusini dhidi ya SuperSport United uliomalizika kwa sare ya bao 1-1.

Mamelodi ni moja ya timu tishio kwa sasa kwenye michuano mbalimbali barani Afrika ikiwa imeanza mwaka vizuri kwa kuchukua Kombe la African Football League baada ya kushinda fainali dhidi ya Wydad Casablanca.

Dkt. Jingu: Kiwango maambukizi ya Malaria Nchini kimepungua
Wafadhili wasababisha sitisho msaada wa chakula