Mgomo wa madaktari katika Hospitali za Umma kote Nchini Kenya, umeanza rasmi hii leo Machi 14, 2024, huku baadhi ya jamaa wakilazimika kuwaondoa wagonjwa wao katika Hospitali hizo, ili kutafuta huduma za matibabu kwingine.
Hata hivyo, shughuli za kawaida katika Hospitali kuu ya Rufaa na Mafunzo ya Kilifi zimeendelea, hivyo kukinzana na tamko la Muungano wa Madaktari ukanda wa Pwani – KMPDU, la mgomo wa Madaktari.
Mmoja wa wauguzi aliyeongea kwa sharti la kutotaja jina, amesema wanaendelea na kazi ya kuhudumia wagonjwa kama kawaida, baada ya uongozi wa madaktari Kilifi kufanya mkutano na Serikali ya Kaunti ya Kilifi.
Muungano wa Madaktari, Wafamasia na Madaktari wa Meno nchini Kenya – KPMDU, ulitangaza mgomo wakiishinikiza Serikali kutimiza mahitaji yao muhimu, ikiwemo kurejeshwa kwa makato ya ushuru wa Nyumba yaliyofanyika katika mishahara yao, ambayo Mahakama ilitangaza kuwa yanafanyika kinyume na Katiba.