Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Damas Ndumbaro, amesema Serikali itakutana na uongozi wa Shirikisho la Sopka nchini Tanzania ‘TFF’, klabu za Simba SC na Young Africans kuona inatoa mchango gani kuhakikisha timu hizo zinafanya vizuri hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kusonga mbele.
Dk. Ndumbaro ameyasema hayo jijini Dar es salaam katika mjadala wa ‘Mwananchi Space’, wenye mada isemayo ‘Ipi nafasi ya Simba, Yanga’ katika vita ya kusaka nafasi ya kufuzu Nusu Fainali Ligi ya Mabingwa Afrika.
Waziri Ndumbaro amesema juma lijalo anatarajia kukutana na TFF, Simba SC, na Young Africans ili kuona wanatoa mchango gani kuhakikisha wanafika hatua za mbele.
“Serikali tunataka kukaa na Simba SC, Young Africans na TFF, ili watuambie tunatakiwa kutoa mchango gani timu kushinda Robo Fainali na zingie nusu fainali. Tunaweza kukutana Jumanne ya juma lijalo”
Waziri huyo amesema pamoja na mambo mengine, Mashabiki wametakiwa kuacha kuwapokea wageni na wafahamu mechi hizo za Robo Fainali ni kufa au kupona na kinachotakiwa ni kuhakikisha timu za Tanzania zinashinda.
Amesema Serikali itakula sahani moja na Mashabiki wa Simba SC na Young Africans ambao wataenda kupokea wageni uwanja wa ndege na kuwasapoti.
“Watanzania niwaombe sana najua kuna utani wa jadi, lakini katika mechi ijayo ili kupanga mikakati, mechi hizi za Robo Fainali ni mechi za kufa au kupona, hatutegemei kuona Mtanzania yeyote akienda kupokea wageni uwanja wa ndege, ama kuvaa jezi za timu za wageni.” amesema Dk. Ndumbaro.
“Kwa hiyo wewe Mtanzania ambaye utakuwa kimbelembele kwenda kupokea wageni uwanjani wa ndege, kuwasapoti kwa namna yeyote, hatutakuelewa na tutadili na wewe kwa vile ambavyo tunaona inafaa,” amesisitiza
Dk. Ndumbaro amesema Tanzania imekuwa nchi pekee iliyofanikiwa kuingiza timu mbili mwaka huu, lakini ukishapata mafanikio haupaswi kutumia muda mwingi sana kushangilia hayo mafanikio, unatakiwa uangalie unafanya nini kuendelea kupata mafanikio zaidi.