Wakati Mashabiki na Wanachama wa Simba SC wakichekelea baada ya kusikia mabosi wa klabu hiyo wamepeleka ofa yao mezani mwa Azam FC ili kumsajili Prince Dube kwenda kutatua tatizo lililopo eneo la ushambuliaji la timu hiyo mambo yameanza kupata ugumu kidogo.
Uwezekano wa Dube kuchezea moja kati ya timu zilizopeleka ofa mezani kwa Azam FC, yaani Simba SC au Al Hilal ya Sudan una ugumu kama mchezaji huyo atasimamia alichowaambia rafiki zake wa karibu.
Juzi Alhamis (Machi 14) usiku, Azam FC ilitangaza kupokea ofa kutoka kwa klabu hizo mbili ikaweka wazi kuwa imeziruhusu rasmi kuendelea na mazungumzo na Dube aliyeandika barua hivi karibuni kutaka kusitisha mkataba na klabu hiyo ya Chamazi, lakini yenyewe ikamkomalia ikitaka afuate masharti ya mkataba.
Mmoja wa marafiki wa karibu wa staa huyo aliyerudisha hadi nyumba na vifaa vyote vya Azam Fc, amesema kwamba baada ya kusikia ofa hizo mbili, mchezaji huyo hajaonyesha kuvutiwa na inaonekana akili yake iko sehemu tofauti kabisa ingawa lolote linaweza kutokea.
Habari zinasema kwamba akili ya staa huyo pamoja na watu wanaomsaidia inaonekana iko zaidi kwa Young Africans ambayo anaisubiri ipeleke ofa mezani na baadhi ya klabu za kwao Zimbabwe ikiwemo Highlanders iliyomuuza kwa Azam mwaka 2020.
“Dube hitaji lake kwa hapa nchini ni Young Africans na anaamini itapeleka ofa mezani ya kuhitaji huduma yake na kinyume na hapo amepanga kujiunga na timu ambayo iko nje ya Tanzania.
“Kwa Simba SC wanahitajika kumshawishi sana ili abadilishe mawazo na kujiunga nayo vinginevyo sio jambo rahisi” kimesema chanzo hicho na kuongeza kuwa Young Africans wako tayari kuweka mezani Shilingi 510 milioni ambalo ndilo dau Azam FC ililomsainishia Dube mwaka jana wakati anaongeza mkataba.
Azam FC wao wanakomaa wanataka Sh700 milioni na wanasema kwamba Simba SC na Al Hilal wamekidhi matakwa yao bila kufafanua kiundani.
Inaripotiwa kuwa uongozi wa Simba SC upo tayari kulipa kiasi cha Dola 300,000 ambacho Azam FC inakihitaji ili kumuachia Dube, japo italipa kwa awamu na upo tayari pia kumlipa mshahara ambao nyota huyo anahitaji ili iweze kumnasa na kuimarisha safu ya ushambuliaji ambayo kwa sasa inaongozwa na Freddy Michael na Omar Jobe.
Azam FC inathibitisha kwamba imepokea ofa kutoka klabu mbili tofauti zikimhitaji mchezaji wetu, Prince Dube, raia wa Zimbabwe. Ofa hizo zimetoka katika klabu za Simba ya Tanzania na Al Hilal ya Sudan. Uongozi unazifanyia tathmini ofa hizo ili kuona ipi inafaa.
Aidha, Azam FC inavikaribisha klabu zingine kuleta ofa zao, kwani milango bado iko wazi,” ilifafanua taarifa ya Azam FC ingawa imegahamika kuwa mchezaji huyo ameshawaambia hadi viongozi kwamba hataenda kwenye klabu hizo mbili.