Eva Godwin – Dodoma.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema Mkoa wake unatarajia kuanzisha Shule zinazotumia lugha ya Kiingereza kufundishia masomo ya Kitaaluma, kwa ajili ya Wanafunzi wanaotoka kwenye familia za kipato kidogo.
Akizungumza na Dar24 Media jijini Dodoma, Chalamila amesema dhumuni la kuanzisha shule hizo ni kuhakikisha Watoto wanaingia katika ushindani wa Kimataifa.
Amesema, “tunajua Lugha yetu ya kiswahili ndio tuliyozaliwa nayo na tumeikuta na tunaipenda sana, lakini lugha ya Kimataifa ambayo kila mtu anapaswa kuijua ni Kiingereza, kwahiyo tunataka kuhakikisha Wananchi wenye hali ya chini pia wanasoma shule hizi.”
“Na tu kifanya namna hiyo tutawafanya watoto wetu wa kitanzania kuingia kwenye ushindani wa shule za Nje ya Nchi, na hii itaendelea zaidi kuboresha elimu katika Nchi yetu,” aliongeza Chalamila.
Hata hivyo, amesema wapo jijini Dodoma kama Kamati kuwasilisha vipaumbele vyao, ili kupata fedha itakayoboresha maendeleo ya miradi mbalimbali ya kimaendeleo, ikiwemo Viwanda, Hospitali, Shule, Barabara nk.
“Dar es salaam ni Mkoa ambao unawatu wengi, na ni mkoa unaoendelea kupanuka, kwahiyo bajeti inalenga katika kupunguza mabadiliko ya tabianchi hasa kwa wale wenye kipato kidogo,” amesema Chalamila