Kikosi cha Ihefu FC, kitaweka kambi jijini Arusha kwa ajili ya kuweka kambi kujiandaa na michezo inayokuja ya Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’.

Timu hiyo imeamua kwenda Arusha baada ya kupoteza mechi zake mbili za Ligi Kuu, ikifungwa mabao 5-0 dhidi ya Young Africans, Machi 11, Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es salaam na bao 1-0 dhidi ya Coastal Union, Machi 14, Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.

Ofisa Habari wa klabu hiyo, Peter Andrew, amesema wanaelekea Arusha si kwa sababu zingine zozote bali ni kwa ajili ya urahisi wa kupata mechi za kirafiki tofauti na kama wangepiga kambi Singida.

“Singida ni nyumbani, lakini kama unakumbuka tuliweka kambi Arusha kwa muda kipindi tunajiandaa na mechi za mzunguko wa pili wa Ligi Kuu, Singida si kama ni sehemu mbaya ya kufanya maandalizi, ila kule Arusha tuna nafasi pana ya kupata michezo ya kirafiki, kuna timu nyingi za daraja la kwanza, Mbuni FC na TMA, kwa hiyo tunaweza kupata mechi mbili tatu, kitu ambacho kinatupa ugumu sana tukiwa hapa, hakuna timu za madaraja ambayo yanaweza kutupa changamoto,” amesema ofisa habari huyo

Ameitaja sababu nyingine ni kwamba wana mechi nyingi watazocheza nje ya uwanja wao wa nyumbani, hivyo wanakwenda ugenini ili kuzoea mazingira pia.

“Kitu kilichopo ni kwamba tuna michezo mingi ya ugenini, kwa hiyo tunakwenda Arusha ili kupata uzoefu zaidi ya kucheza ugenini, baada ya hapo tutaanza kuzunguka kuanzia Dar es salaam na sehemu zingine, tukimaliza mechi hizo ndiyo tunarudi kujikita nyumbani Singida,” amesema Peter.

Ihefu hivi sasa imehamia mkoani Singida na inacheza mechi zake kwenye Uwanja wa Liti, Singida, huku ikipishana na Singida Fountain Gate ambayo imehama mkoani humo ikielekea Mwanza, na kupiga mechi zake za Ligi Kuu, Uwanja wa CCM Kirumba jijini humo.

Timu hiyo ipo nafasi ya 11 ya msimamo wa Ligi Kuu, ikiwa na alama 23 mpaka sasa.

Kampuni za uchimbaji wa Mafuta, Gesi zakaribishwa Zanzibar
Michael Jackson afunga ndoa na Sony, atishia kuondoka