Nahodha wa Simba SC, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ amesema chini ya Kocha Abdelhak Benchikha anaamini wataifunga Al Ahly na kutinga Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mchezo wa mkondo wa kwanza kati ya Simba SC na Al Ahly umepangwa kuchezwa Ijumaa (Machi 29), mwaka huu Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Nahodha huyo amesema dhamira yao pamoja na mbinu bora kutoka kwa Kocha Mkuu, Benchikha ndio vinavyompa matumaini.
“Ni kweli Al Ahly ni timu kubwa na ina uzoefu mkubwa kwenye hatua hizi lakini Simba tuna kocha mkubwa anayewajua vyema wapinzani, naamini mbinu zake na kujituma kwao ndio mafanikio,” amesema Tshabalala.
Nahodha huyo ameeleza kuwa wao kama wachezaji wamedhamiria kuumaliza mchezo huo nyumbani kwa kushinda idadi kubwa ya mabao.
Amesema wanawajua vyema wapinzani wao sababu wameshakutana nao kwenye michuano ya AFL na kutoka sare katika mechi zote mbili hivyo wa wanapo pakuanzia.
Simba SC imepangwa na Al Ahly baada ya kumaliza nafasi ya pili kwenye mechi za hatua ya makundi ya michuano hiyo na safari hii imedhamiria kufika hatua ya Nusu Fainali.