Baada ya kupata ushindi wa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Jumapili (Machi 17) dhidi ya Young Africans, Klabu ya Azam FC imeonekana kubadili malengo na sasa imekuja na kauli nyingine kuwa wanautaka ubingwa wa Tanzania Bara.
Hivi karibuni klabu hiyo ilidai kunyoosha mikono kwenye mbio hizo ikisema inajipanga kwa msimu ujao, lakini ushindi huo umeifanya ghafla kubadili gia angani.
Ofisa Habari wa Klabu ya Azam, Hasheem Ibwe, amesema kuwa bado wapo sana kwenye mbio za kuusaka ubingwa wa Tanzania Bara na haijalishi michezo mingi waliocheza dhidi ya timu zingine.
“Bado sisi tupo kwenye mbio za ubingwa kwa sababu ni moja kati ya timu mbili za juu, haijalishi michezo ambayo tumecheza au wenzetu hawajaifikia, tumeshawahi kuona timu zikiwa na michezo mingi, lakini zinapoteza mchezo mmoja na kuwavunja nguvu kuelekea kwenye mechi zingine na kujikuta zinapoteza pia, kwa hiyo bado tunaanmini tupo kwenye mbio hizo, na ukitaka ubingwa ni lazima uzifunge timu kubwa kama Young Africans,” amesema Ibwe.
Akizungumzia jinsi walivyoupokea ushindi dhidi ya Young Africans, amesema ulikuwa wakati mzuri kwao baada ya muda mrefu heshima yao kupotea kwa kutoweza kupata matokeo mazuri dhidi ya timu hiyo.
“Ulikuwa ni wakati mzuri sana upande wetu kwa sababu tulipata ushindi na kikubwa zaidi ni jinsi vijana wetu walivyokuwa wamejitoa kwenye ule mchezo ili kurudisha heshima yetu ambayo klabu yetu ilikuwa ikiikosa kwa muda mrefu sasa.”
“Kwa niaba ya Klabu ya Azam, tunawapongeza watu wote, wachezaji na benchi la ufundi, waliokuwa nyuma yetu na kutuombea, hata waamuzi ambao walikuwa kwenye kiwango bora siku hiyo,” amesema.
Matokeo ya mechi hiyo yameifanya timu hiyo kukaa kwenye nafasi ya pili ikiwa na alama 47, chini ya alama tano kwa vinara Young Africans, na moja juu ya Simba SC iliyo katika nafasi ya tatu ya msimamo.