Arsenal imetikiswa baada ya beki wake mahiri kabisa, Gabriel kujiondoa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Brazil baada ya kudaiwa anasumbuliwa na maumivu.
Beki huyo wa kati alitarajia kuanza kwenye mechi ya Jumamosi (Machi 23) dhidi ya England itakayopigwa huko Wembley akiwa na kikosi cha Brazil maarufu kama Samba Boys.
Hata hivyo, alifanya mazoezi kidogo kwenye kambi ya timu ya taifa ya Brazil iliyopo kwenye viwanja vya mazoezi ya Arsenal, London Colney, lakini aliondolewa kwa kikosi ili asiumie zaidi baada ya kuonekana kuwa na tatizo.
Maumivu hayo mapya hayahusiani na yale ya mguu ambayo yamekuwa yakimsumbua Gabriel kwa siku za karibuni.
Kocha wa Brazil, Dorival Junior alisema beki huyo ameondolewa kwenye kikosi cha nafasi yake kuchukuliwa Bremer kutoka Juventus.
Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta anataka kumlinda beki wake hadi hapo mapumziko ya mechi za kimataifa za kirafiki zitakapopita na kurudi uwanjani kwenye Ligi Kuu England kuwakaribisha Man City, Machi 31.
Amecheza mechi 26 kwenye Ligi Kuu England msimu huu, akiunda kombinesheni matata kabisa na William Saliba, kuifanya Arsenal kuwa na ukuta mgumu kabisa, ikiwa imeruhusu mabao 24 tu.
Gabriel mwenye umri wa miaka 26, ameungana na kundi dogo la wachezaji majeruhi kwenye kikosi cha Arsenal, sambamba na Gabriel Martinelli, ambaye pia hakuitwa kwenye kikosi cha Brazil.
Thomas Partey naye hakujiunga na Ghana kwa kuwa bado hajapona vyema na Jurrien Timber anapambana na muda kupona haraka.
Baada ya mechi ya Man City, Arsenal itakipiga na Luton na Brighton kabla ya kurusha kete yake ya kwanza kwenye mchezo wa Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Bayern Munich, Uwanja wa Emirates.