Kocha wa Azam FC, Yossouph Dabo, amesema kikosi chake kinakabiliwa na mechi tano ngumu ambazo anahitaji kushinda kwa lengo la kuzidi kujivweka katika nafasi nzuri ya kutwaa Ubingwa msimu huu 2023/24.
Mechi hizo ni dhidi ya Simba SC, Ihefu FC, Namungo FC, Mtibwa Sugar na KMC.
Azam FC imebakiza michezo tisa kabla ya kumaliza Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kucheza mechi 21 na kujizolea alama 47, ikiwa nafasi ya pili.
Akizungumza jijini Dar es salaam, Dabo amesema pamoja na mechi zote zilizobaki kuwa ngumu, anaumiza kichwa zaidi na michezo mitano inayofuata.
Dabo amesema katika mechi hizo, kikosi chake kinahitaji walau alama 12 kati ya 15 kwa lengo la kujihakikishia nafasi ya mbio za kuwania taji.
Amesema pamoja na ushindani mkali katika michezo ya lala salama, atahakikisha anakipanga kikosi chake kutoa upinzani na kushinda michezo yote iliyobaki.
“Tuna mechi tano za moto ambazo tunahitaji ushindi wa hali na mali pamoja na kuwa mechi zote zilizobaki zina umuhimu, naendelea kuiandaa timu kufanya maajabu mengine kama tulivyofanya katika mchezo uliopita dhidi ya Young Africans,” amesema.
Kocha huyo amesema katika kipindi hiki cha lala salama, atahakikisha timu yake inapambana bila kuchoka huku ikiweka lengo la kutwaa ubingwa hata kama wapinzani wao wamejipanga kutetea kwa mara nyingine.
Juzi Jumamosi (Machi 23), Azam ilipata ushindi wa mabao 2-1, katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Zimamoto, uliochezwa Azam Complex.
Ligi Kuu itakaporejea, Azam FC itakuwa na Kibarua dhidi ya Namungo FC mchezo utakaochezwa April 13, mwaka huu Uwanja wa Majaliwa, Lindi.