Beki wa kati wa Barcelona, Ronald Araujo, amesisitiza kuwa bado ana furaha katika klabu hiyo, akipuuza ripoti kwamba anaweza kuondoka msimu huu wa majira ya joto.
Wakati Araujo akibakia kuwa mchezaji muhimu wa Barcelona, imependekezwa kuwa anaweza kuuzwa msimu huu wa majira ya joto ili kukusanya kiasi kikubwa cha fedha, huku timu kama Bayern Munich na Manchester United zikipigiwa upatu kuwasilisha ombi la kumnunua mchezaji huyo wa Kimataifa wa Uruguay.
Hata hivyo, Araujo ameamua kuweka uvumi huo wazi, akisisitiza furaha yake na maisha ya Barcelona.
“Kumekuwa na mazungumzo mengi kuhusu hili, lakini nina furaha Barcelona,” alisema akiiambia La Quinta Tribuna.
“Mbali na hilo, tunapaswa kumaliza msimu vizuri kwa sababu bado kuna changamoto mbeleni, ikiwa ni pamoja na Copa America.”
Kinachochochea moto wa uwezekano wa kuondoka ni ukweli kwamba mkataba wa sasa wa Araujo unatarajiwa kumalizika 2026 na huenda Barcelona wasiweze kushindana na aina ya mishahara ambayo atapewa kwingineko.
Rais wa Klabu Joan Laporta, ambaye hapo awali alikiri kuwa atamfunga Araujo kwa mkataba wa maisha ikiwezekana, hivi karibuni alikiri kumekuwa na vikwazo katika mazungumzo na wawakilishi wa beki huyo wa Ekati, lakini akasisitiza masuala yote sasa yameshughulikiwa.