Timu ya Tabora United imemtambulisha, Masoud Djuma kuwa kocha msaidizi wa timu hiyo akisaidiana na Kocha Mkuu, Denis Goavec raia wa Ufaransa.
Akizungumza Mtendaji Mkuu wa timu hiyo, Thabiti Kandoro amesema wamempa kocha huyo mkataba wa mwaka mmoja sawa na bosi wake Goavec na hiyo ni kutokana na kuvutiwa na utendaji wake kote alikopita.
Mtendaji huyo amesema wameamua kulisuka upya benchi la ufundi kwakuwa malengo yao ni kuiona Tabora United ikifanya vizuri kwenye Ligi Kuu na kufikia malengo ambayo wameyakusudia msimu huu.
Amesema kwakuwa huu ndio msimu wa kwanza kushiriki ligi, lengo lao sio ubingwa bali ni angalau kuwemo kwenye nafasi tano za juu na kwa aina ya usajili walioufanya msimu huu anaamini hilo linawezekana.
Tabora United imeajiri makocha wapya baada ya kuachana na Goran Kopnovic, raia wa Serbia ambaye ndiye alikuwa Kocha Mkuu lakini walishindwa kuendelea naye kutokana na mwenendo mbaya wa timu hiyo kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.
Timu hiyo ipo nafasi ya 13 kwenye msimamo wa ligi ikiwa na alama 23 katika michezo 21 ambayo wamecheza hadi sasa na imebakiwa na michezo tisa kabla msimu kumalizaka.