Msemaji wa Jeshi la Polisi Nchini, DCP David Misime amesema Polisi wanafuatilia tukio la kufyatuliwa risasi kwa Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka na Dereva wake wakati wakiwa safarini tukio lililotokea katika Kijiji cha Ngabolo kilichopo Wilayani Kiteto Mkoani Manyara.
Misime ameyasema hayo na kuongeza kuwa wanafuatilia tukio hilo kwa ukaribu na uchunguzi ulishaanza mara tu baada ya kupokea taarifa.
Amesema, “Timu ya Wataalamu wa uchunguzi wa matukio na matumizi ya risasi kutoka Makao Makuu ya Polisi Dodoma imetumwa kwenda kushirikiana na Timu ya Mkoa wa Manyara kuchunguza tukio hilo.”
“Ushirikiano huo unalenga kubaini waliohusika ni akina nani na madhumuni au kusudio lao lilikuwa ni nini na baada ya uchunguzi wa Wataalamu taarifa kamili itatolewa,” amesema DCP Misime.
Katika tukio hilo, watu wasiojulikana walimfyatulia risasi zisizopungua nne Mbunge huyo wa Simanjiro akiwa ndani ya gari lake sna Dereva wake majira ya saa moja usiku Machi 29, 2024 na kisha kukimbia muda mfupi baada ya Mbunge huyo naye kuanza kupiga risasi juu kuwatishia.
“Ni kweli nimeshambuliwa kwa risasi majira ya saa moja kasoro katika Wilaya ya Kiteto kati ya Kijiji cha Ngabolo na Ndedo, kulikuwa na gari ambayo ilikuwa inanifuatilia kwa nyuma tukawapisha kidogo kama tunataka kuwapisha wapite kulia walipofika usawa wetu wakaanza kumimina risasi kwa Dereva na baada ya hapo wakavuta kwenda mbele halafu wakaanza kuzipiga za usoni na sisi tukakata kona kugeuza na Mimi nikaanza kupigapiga (risasi) za juu pale kuwatishiatishia ndio tukafanikiwa kugeuza na kuondoka.” alisimulia Ole Sendeka.
Amesema, “walikua na silaha kubwa na silaha ndogo, hakuna aliyepata madhara tulikuwa Mimi na Dereva wangu ni gari tu ndio wameichakazachakaza wameipigapiga, mpaka sasa kwakuwa tumekuja gizani huku hatujazihesabu lakini zipo risasi moja, mbili, tatu, nne kama nne hivi hatujazihesabu.”