Kocha mpya wa Tabora United, Denis Goavec, amesema baada ya muda mfupi tu kuwapo ndani ya kikosi hicho, amegundua mambo kadhaa ambayo anadhani yalikuwa yakisababisha timu hiyo isifanye vizuri katika mechi zake za Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kocha huyo raia wa Ufaransa aliyechukua nafasi ya Mserbia, Goran Copunovic, amesema hakukuwa na nidhamu kwa wachezaji, ambapo pia hawakuwa na furaha kikosini.
“Nilichokutana nacho kwanza kabisa nidhamu kwa wachezaji ilikuwa ndogo, halafu walikuwa hawana furaha, siwezi kujua ni kwa sababu gani ilikuwa hivyo kabla ya sisi kufika.”
“Kazi yangu kubwa iliyopo kwa sasa ni kurudisha nidhamu na furaha kwa wachezaji, kama hivyo vyote vikiwepo basi kila kitu kinawezekana,” amesema kocha huyo.
Amesema kwa sasa anakiandaa kikosi chake kwa ajili ya mechi ya Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ itakayochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jjini Mwanza, Kweshokutwa Alhamis (Aprili 4) dhidi ya Singida Fountain Gate.
“Itakuwa mechi nzuri kwetu, hatutokuwa tayari kushindwa na ndiyo mechi itakayorejesha furaha ya mashabiki wa Tabora United,” amesema Goavec.
Timu hiyo inashika nafasi ya 13 ikiwa na pointi 21, ikicheza mechi 21, kushinda nne, sare tisa na kupoteza nane.
Awali, mara tu baada ya kupewa timu, kocha huyo alidai kugundua shida kwenye safu yake ya ushambuliaji pamoja na viungo watengeneza nafasi.
“Nimeangalia kitu na nimegundua safu ya ushambuliaji ina shida, tumetengeneza nafasi chache na tumefunga mabao machache, kwa hivyo lazima kwanza tuanze na yale mapungufu makubwa ambayo nimeyagundua baada ya kufuatilia mechi kadhaa ilizocheza huko nyuma,” alisema kocha huyo.
Timu hiyo imefunga mabao 15 mpaka sasa na kuruhusu 25, ikiwa imesalia na mechi tisa tu za Ligi Kuu msimu huu 2023/24.