Watanzania wametakiwa kuepuka matumizi ya Dawa za Kulevya kwani yanaharibu nguvukazi ya Taifa hasa vijana ambao wanategemewa kuongoza kufanya shughuli za uzailishaji na kuharakisha maendeleo.
Wito huo, Umetolewana Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa katika sherehe za uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru zilizofanyika kitaifa Katika Viwanja vya Chuo cha Ushirika Moshi Mkoani Kilimanjaro.
Amesema, “idadi kubwa ya waathirika wa matumizi ya dawa za kulevya ni watoto na vijana wenye umri kati ya miaka 13 hadi 24. Kundi hili ni nguvukazi ya Taifa letu, Serikali, haiwezi kunyamaza itaendelea kufanya msako mkali ili wahusika wote wa biashara hiyo haramu wachukuliwa hatua kali.”
Majaliwa ameongeza kuwa, Serikali kwa kutambua umuhimu wa udhibiti wa biashara ya dawa ya kulevya imeendelea kuongeza kasi ya mapambano ili kukomesha biashara, kilimo na matumizi ya dawa za kulevya. “Hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wote wanaojihusisha na kilimo hicho haramu pamoja na biashara ya dawa za kulevya.”
“Viashiria vya kuwepo kwa ongezeko la matumizi ya dawa za kulevya nchini ni pamoja na kuongezeka kwa idadi kubwa ya watumiaji wanaotafuta matibabu, kuongezeka kwa watu wanaokamatwa wakitumia dawa za kulevya, kiasi cha dawa za kulevya zinazokamatwa zikiingizwa nchini na kuwepo kwa uhalifu unaohusishwa na matumizi ya dawa za kulevya hasa uporaji, wizi na ukabaji,” amesema Waziri Mkuu.
Aidha, amesema mbio za mwenge wa uhuru za mwaka 2024 zitaendelea kutoa hamasa kwa jamii kusitisha kilimo haramu cha bangi, biashara na matumizi ya dawa za kulevya. Aidha, utajiekeleza kwenye kuhamasisha jamii kulima kilimo cha mazao halali ya biashara na chakula, pamoja na kuhamasisha jamii kushiriki katika shughuli nyingine halali na zenye staha.