Wakati Simba ikikutana na mwamuzi wa nuski kwao aliyepangwa kuchezesha mchezo wa ugenini wa hatua ya Robo Fainali dhidi ya Al Ahly kesho Ijumaa (Aprili 05), watani wao wa jadi Young Africans wamepangiwa refa aliye na bahati kwao watakapokabiliana na Mamelodi Sundowns ugenini.

Mchezo wa Al Ahly dhidi ya Simba SC ambao utakuwa katika Uwanja wa Kimataifa wa Cairo, Misri umepangiwa mwamuzi Alhadi Allaou Mahamat kutoka Chad ambaye amekuwa hana historia nzuri kwa timu za Tanzania.

Katika mechi hiyo, Simba SC inahitaji ushindi wa zaidi ya bao moja ili iweze kutinga hatua ya Nusu Fainali baada ya kupoteza kwa bao 1-0 katika mechi ya kwanza nyumbani wiki iliyopita.

Mwamuzi huyo mwenye umri wa miaka 37, ndiye alichezesha mechi ambayo Simba SC ilipoteza kwa mikwaju ya penalti 4-3 dhidi ya Wydad ugenini msimu uliopita ambayo ilikuwa ya marudiano ya hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, baada ya Wydad kupata ushindi wa bao 1-0 katika dakika 90 za mchezo.

Mahamat pia alichezesha mechi ambayo timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ ilipoteza kwa mabao 3-0 dhidi ya Morocco katika mchezo wa hatua ya makundi ya Fainali za Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’ zilizofanyika Ivory Coast mwanzoni mwa mwaka huu.

Ikumbukwe pia ndiye refa alisimama katikati kuchezesha mechi ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika msimu huu ambayo Young Africans ilipoteza kwa mabao 3-0 mbele ya CR Belouizdad ya Algeria, Novemba 24, mwaka jana.

Sio aina ya refa ambaye amekuwa akipendelea kumwaga sana kadi na kuthibitisha hilo, katika mechi 19 za mashindano ya klabu Afrika ambazo amechezesha, ameonyesha idadi ya kadi 66 sawa na wastani wa kadi tatu kwa mechi.

Mshambuliaji wa zamani wa Simba SC, Musa Hassan ‘Mgosi’ amesema kuwa timu hiyo haipaswi kumfikiria refa wa mchezo.

“Hatua kama hizi ni kubwa kwenye mashindano hivyo refa hawezi kuchezesha vibaya ili kupendelea wenyeji. Wachezaji wa Simba SC wanapaswa kufanyia kazi kile ambacho Benchi la Ufundi litawaelekeza na sio kumfikiria refa. Refa hawezi kuionea timu ambayo iko bora ndani ya uwanja hivyo naamini atatenda haki kwani ni refa mkubwa,” amesema Mgosi.

Wakati hali ikiwa hivyo kwa Simba SC, mchezo wa marudiano wa hatua ya Robo Fainali Ligi ya Mabingwa Barani Afrika baina ya Mamelodi Sundowns na Young Africans utakaochezwa kesho Ijumaa (Aprili 05), Pretoria, Afrika Kusini utachezeshwa na Beida Dahane kutoka Mauritania mwenye historia nzuri na Young Africans.

Refa huyo mwenye umri wa miaka 32 ndiye alichezesha mechi ya Mkondo wa Pili wa hatua ya Fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika msimu uliopita ambao Young Africans iliibuka na ushindi wa bao 1-0 lililotokana na mkwaju wa Penati wa Djuma Shaban, ambao mwamuzi huyo aliamuru baada ya mmoja wa walinzi wa USM Alger kufanya kosa ndani ya eneo la hatari la timu yake.

Miezi minne baadae, Dahane ambaye alipata beji ya kimataifa ya urefa kutoka Shirikisho la Soka Duniani ‘FIFA’ mwaka 2018 alichezesha mechi ya marudiano ya Raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika ambayo Singida Big Stars ya Tanzania ilichapwa mabao 4-1 na Future ya Misri.

Hersi: Timu ipo tayari kupambana Afrika Kusini

Lakini pia Dahane ndiye alichezesha mechi ya kwanza ya hatua ya Robo Fainali ya mashindano ya African Football League (AFL) ambayo Simba SC ililazimishwa sare ya mabao 2-2 nyumbani na Al Ahly, Oktoba 20 mwaka jana.

Katika mechi hiyo dhidi ya Mamelodi ambayo itachezwa kwenye Uwanja wa Loftus Versfeld, Young Africans inahitaji ushindi au sare ya aina yoyote ya mabao ili iweze kusonga mbele baada ya timu hizo kutoka sare tasa katika mechi ya kwanza, Jumamosi iliyopita (Machi 30) jijini Dar es salaam.

Majanga mazito Manchester United
Singida Black Stars yaanika malengo yake