Kocha Mkuu wa Simba SC, Abdelhak Benchikha, amesema dhamira yao ni kuleta furaha kwa mashabiki kwa sababu wana nafasi ya kufanya vizuri, dhidi ya Al Ahly katika mchezo wa Mkondo wa Pili wa Robo Fainali, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.

Simba SC itacheza ugenini Cairo, Misri kesho Ijumaa (Aprili 05) katika Uwanja wa Cairo International Stadium, huku ikiwa na deni la kupoteza mchezo uliopita kwa 0-1, Uwanja wa Benjamin mkapa jijini Dar es salaam juma lililopita.

Benchikha amesema mbali na ubora wa Al Ahly, timu hiyo inafungika kwa kuwa wataingia uwanjani na mbinu bora za kupata matokeo mazuri.

Kocha huyo amesema atatumia uzoefu wake katika mechi za kimataifa kupata ushindi, kwa sababu ana kikosi bora cha wachezaji hodari.

“Malengo yetu Simba SC ni kwenda Nusu Fainali, tulipoteza kwa makosa washambuliaji walikosa umakini lakini tumerekebisha ili tupate matokeo mazuri ugenini na hilo linawezekana,” amesema Benchikha.

Beki na Nahodha Msaidizi wa Simba SC, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, amesema watapambana kufa au kupona kushinda mchezo huo.

“Huu ni mchezo muhimu kwetu, utatuonyesha dira ya kusonga mbele katika mashindano haya, tutapambana na tutafuata ambacho mwalimu ametufundisha ili kupata ushindi,” amesema

Simba SC ilitinga Robo Fainali baada ya kushika nafasi ya pili katika Kundi B ikiwa na pointi tisa, nyuma ya kinara ASEC Mimosas ya lvory Coast iliyovuna pointi 11.

Al Ahly iliongoza Kundi D kwa pointi 12 baada ya kucheza mechi sita, ikifuatiwa na Young Africans iliyomaliza kwa pointi nane.

Mara ya mwisho Simba SC kucheza Nusu Fainali ya michuano hiyo ilikuwa mwaka 1974, wakati huo ikifahamika Klabu Bingwa Afrika, ilifungwa na Mehalla El Kubra ya Misri kwa Penati 3-0 baada ya kutoka sare kufuatia kila mmoja kushinda nyumbani bao 1-0.

Afariki kwa kudondokewa na ukuta Moro
Wachezaji Young Africans wala kiapo Afrika Kusini