Mbivu na Mbichi ya timu za Tanzania kwenda hatua ya Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika inatarajiwa kujulikana usiku wa leo Ijumaa (Aprili 05), zitakapokuwa ugenini kupeperusha bendera ya nchi katika mechi zao za marudiano hatua ya Robo Fainali.

Mabingwa wa nchi, Young Africans wapo nchini Afrika Kusini, ambapo wao wataanza kushuka kwenye dimba la Loftus Versfeld kucheza dhidi ya Mamelodi Sundowns ya huko, mchezo utaopigwa saa 3:00 usiku wa saa za Afrika Mashariki.

Wawakilishi wengine wa Tanzania, Simba SC wataingia uwanjani baadae, saa 5:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki, kuwavaa Mabingwa Watetezi wa kombe hilo, Al Ahly ya Misri, mchezo ukichezwa Uwanja wa Kimataifa wa Cairo.

Mechi zote ni za marudiano baada ya zile zilizochezwa ljumaa na Jumamosi iliyopita Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam.

Katika mechi iliyochezwa ljumaa iliyopita (Machi 29), Simba SC ilipoteza kwa bao 1-0, hivyo ina kazi kubwa ya kulipa kisasi na kuweza kusonga mbele ya michuano hiyo mikubwa Barani Afrika.

Ili kusonga mbele, Simba SC inatakiwa kushinda kuanzia mabao mawili au ushindi mwingine zaidi ya huo, lakini idadi ya mabao iwe inawazidi wenyeji bao moja au zaidi ya hapo.

Kocha Mkuu, Abdelhak Benchikha, amesema kila kitu kimekwenda kama kilivyopangwa, na anaamini vijana wake watatekeleza kile ambacho amewaambia kwenye uwanja wa mazoezi.

“Kazi yetu kubwa ni kushambulia kwa ajili ya kupata bao la mapema na kuwaweka kwenye presha wapinzani wetu ili wasitushambulie kwa mfululizo.”

“Nadhani wachezaji wangu wakifanikiwa kupata bao, mechi itakuwa ngumu kwa wenyeji, hatutokaa nyuma, tutashambulia na kuzuia kwa pamoja,” amesema Benchika.

Mmoja wa wachezaji waandamizi wa timu hiyo, Clatous Chama amekiri ugumu wa mechi ya leo, lakini watapambana kuhakikisha wanasonga mbele.

“Kazi yetu itakuwani kushambulia ili kupata matokeo dakika za mapema licha ya mlima mrefu tulionao, tunategemea mechi itakuwa ngumu kwa dakika zote 90, lakini tumejiandaa kushindana.”

“Kupoteza kwenye uwanja wetu wa nyumbani mechi iliyopita ni sehemu ya matokeo na haitufanyi eti tuingie uwanjani tukiwa tumekubali kushindwa, wenzetu walitufunga nyumbani na sisi tunaweza kuwafunga kwao,” alisema Chama.

Chama amesema katika mechi iliyopita ilionekana hawakuwa na bahati, huku akimsifu kocha Benchika kuwa ni mzoefu hasa anapokuwa kwenye michuano hiyo.

“Tulicheza vizuri uwanja wa nyumbani hatukuwa na bahati tu, tunataka bao la mapema ili kuturudisha kwenye ushindani.”

“Tuna kocha mwenye uzoefu ambaye ametoka kutwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika ukichanganya na wachezaji wazoefu tuliopo ambao tumepata nafasi ya kucheza hatua ya Robo Fainali zaidi ya misimu mitatu, kuna kitu kitaongezeka,” amesema kiungo huyo raia wa Zambia.

Gamondi atamba kuishangaza Afrika
Wakutana kujadili utekelezaji shughuli za EITI nchini