Kiungo Mshambuliaji wa zamani wa mabingwa wa soka wa Tanzania Bara Young Africans, Sekilojo Chambua amesema amesikitishwa na maamuzi mabovu kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns.
Young Africans ilifungwa kwa mikwaju ya Penati 32 na Mamelodi katika Uwanja wa Loftus Versfeld, Pretoria Afrika Kusini baada ya dakika 90 za mchezo huo kumalizika kwa sare ya bila kufungana.
Kipindi cha pili cha mechi hiyo iliyokuwa na ushindani mkali, mwamuzi kutoka Mauritania Dahana Balde aliinyima Young Africans bao lililofungwa na kiungo wake mshambuliaji Stephan Aziz Ki aliyepiga mpira uliogonga mwamba wa juu na kuingia ndani.
Hata hivyo mwamuzi aliyechezesha mchezo wa fainali ya Mataifa ya Afrika Februari 12 mwaka huu kati ya wenyeji na Ivory Coast na Nigeria, alilikataa bao hilo kwa kigezo kuwa mpira huo haukuvuka mstari na wala hakwenda kuangalia marejeo ya video.
Chamnbua aliyekuwa akimudu vyema nafasi za winga ya kulia, namba nane na 10 amesema timu yake hiyo ya zamani imedhulumiwa ushindi na ni fedheha kwa soka la Afrika.
“Kila mmoja aliona kilichotokea na kila mmoja aliona namna Young Africans walivyoonesha kiwango bora dakika zote mpaka wakafanikiwa kufunga bao la Aziz Ki.”
“Ni wazi mpira wote ulivuka mstari na watu wote waliona, lakini nashangaa kwanini mwamuzi hakuona na wala hakujisumbua kwenda kwenye ‘VAR’.” amesema Chambua
Amesema Young Africans wametolewa kwa mizengwe na kusema wasikate tamaa na badala yake wajipange kufanya vizuri zaidi msimu ujao.