Simba SC leo Jumanne (Aprili 09) itashuka katika Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma kuvaana na Mashujaa FC, kwenye mechi ya 16 bora ya CRDB Federation Cup.

Simba SC itashuka uwanjani ikiwa na kazi ya kutaka kuwafariji wanachama na mashabiki wa timu hiyo ambao wanaonekana kuhuzunika kwa kuchapwa mabao 2-0 dhidi ya Al Ahly ya Misri kwenye Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, katika mechi iliyochezwa ljumaa iliyopita (Aprili 05) Uwanja wa Kimataifa wa Cairo, ikisukumwa nje kwa jumla ya mabao 3-0, kutokana na kufungwa bao 1-0 nyumbani.

Kutokana na kuondolewa kwa michuano hiyo, Simba SC imebakisha mataji mawili ambayo inaendea kupambana nayo kwa ajili kuyatia kibindoni nayo ni kombe hilo pamoja na Ligi Kuu Tanzania Bara, huku ikiwa tayari ina Ngao ya Jamii mkononi iliyoitwaa Agosti 13, ilipowachapa watani zao wa jadi, Young Africans kwa mikwaju ya Penati 3-1, Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.

Simba SC inakwenda kucheza na timu ambayo mara mwisho ndiyo iliyokutana nayo katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es salaam, Machi 15 na kushinda mabao 2-0.

Timu yoyote itakayoshinda itatinga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo ambayo bingwa wake huiwakilisha nchi kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.

Kocha Mkuu wa Simba SC, Benchikha amesema wanakwenda kucheza mechi hiyo muda mfupi tu baada ya kutoka mechi yao dhidi ya Al Ahly tena wakiwa ugenini, hivyo anatarajia kutakuwa na uchovu kwa wachezaji wake, lakini hiyo haiwezi kuwa kisingizio cha kutofanya vizuri kwenye mchezo wa leo.

“Tuna baadhi ya wachezaji ambao hawakucheza mechi ile tutawatumia, lakini pia wapo waliocheza ila watatumika kwa dakika kadhaa au zote kutegemea na mwenendo wa mechi,” amesema

Kocha Mkuu wa Mashujaa FC, Mohamed Abdallah ‘Bares’ amesema kutokana na mazoezi ambayo amewafanyisha vijana wake, anaamini watafanya vizuri katika mechi ya leo Jumanne (Aprili 09).

“Tumekaa muda mrefu bila kucheza mechi yoyote, nadhani mara ya mwisho tulicheza dhidi ya hawa hawa Simba SC, Dar es salaam katika mchezo wa Ligi Kuu, tuliwapa mapumziko mafupi wachezaji wetu, lakini walirejea na kufanya mazoezi ya nguvu kujiandaa na mchezo huu, naamini tutafanya vizuri,” amesema kocha huyo.

Serikali kutoa taarifa tathmini ya Mazingira
Majaliwa: Tuendelee kuuenzi, kuulinda Muungano wetu