Wizara ya Afya, kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo imeandaa kampeni ya Kitaifa ya kutoa chanjo ya kukinga saratani ya mlango wa kizazi kwa wasichana wote walio na umri wa miaka 9 hadi 14.
Akizungumza na Waandishi wa habari katika semina ya mafunzo ya saratani ya mlango wa kizazi iliyofanyika Jijini Dodoma, Mkurugenzi wa kinga kutoka Wizara ya Afya, Dkt.Tumaini Haonga amesema, kampeni hii itafanyika nchi nzima kuanzia April 22 hadi 28, 2024 wakati wa maadhimisho ya wiki ya chanjo Afrika katika vituo vya kutolea huduma za chanjo na shuleni.
Hata hivyo, Dkt. Haonga amewaomba Waandishi wa Habari kuendelea kutoa elimu kwa Umma, kuendelea kufanya uchunguzi wa awali mara kwa mara juu ya saratani ya mlango wa kizazi.
“Zipo sababu mbalimbali ambazo kwa nyakati tofauti tumeendelea kusisitiza lakini kwa magonjwa haya ambayo yanazuilika kwa chanjo ni muhimu tuweke msisistizo mkubwa kwa wananchi kutumia nafasi hii ya kupata chanjo kama nafasi pekee ya kupata kinga ya uhakikaa,” amesema.
”Tuna wananchi ambao kwa bahati mbaya hawajapata fursa ya kufahamu masuala ya msingi kuhusu kanuni muhimu za afya,sasa kundi hili la wananchi wao wanategemea taarifa ,na taarifa wanazipata kutoka kwa wananchi wenzao,taarifa wanazipata kutoka Kwenye mitandao ya kijamii,taarifa watazipata kutoka Kwa wanahabari,” amesema Haonga.
Naye, Mratibu wa chanjo Wizara ya Afya, Lotalis Gadau amesema kuwa utoaji wa chanjo katika kampeni hii utahusisha vituo vya kutolea huduma za Afya,huduma za mkoba,shule na timu za uchanjaji zitakuwa kwenye vituo kwa siku nne.
“Lengo letu ni kuwapa kinga mabinti wa miaka 9 hadi 14 na kuzuia kuenea kwa maambukizi ya saratani ya mlango wa kizazi kwa Wanawake hapo baadae,” amesema.
“Na ni muhimu kwa mzazi au mlenzi kuhakikisha mtoto anakamilisha chanjo zote kulingana na ratiba,chanjo zote ni salama zimethibitishwa na Wizara ya Afya na Shirika la Afya Duniani,” amesema Gadau
Uzinduzi wa chanjo hiyo ya mlango wa kizazi Kitaifa itafanyika Mkoani Mwanza April 22, 2024 ikiwa imebeba kauli mbiu isemayo “JAMII ILIYOPATA CHANJO,JAMII YENYE AFYA”.