Mlinda Lango wa Klabu ya Singida Fountain Gate, Beno Kakolanya, amegoma kuhudhuria kikao cha Kamati ya Utendaji akidai hakitamtendea haki.
Msemaji wa timu hiyo, Hussein Masanza, amesema mlinda mlango huyo aliandikiwa barua ya wito Aprili 15, ikimtaka kuhudhuria kikao cha Kamati ya Nidhamu Aprili 19, mwaka huu, lakini alishindwa kutii wito huo.
“Ni kweli Beno alipewa barua ya wito na Kamati ya Nidhamu ikimtaka ahudhurie kikao ambacho kilipangwa kufanyika Aprili 19, lakini aligoma akidai kamati haitamtendea haki kutokana na tuhuma alizotuhumiwa za kuihujumu timu yao,” amesema Masanza.
Amesema alipaswa kwenda kujibu sababu zilizomfanya atoroke kambini na kuhujumu timu, siku chache kabla ya kukutana na timu ya Young Africans katika mchezo ambao ulichezwa Aprili 14, mwaka huu jijini Mwanza.
Ameongeza kuwa kwa kitendo alichokifanya uongozi utamchukulia hatua kali ili iwe fundisho kwa kuwa ameonyesha utovu wa nidhamu.