Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Aldof Mkenda ametembelea baadhi ya shule zilizoathiriwa na mafuriko Kibiti na Rufiji, kuzungumza na Wanafunzi, Walimu na Wazazi kisha kuagiza wote waliokuwa wakisoma katika Shule zilizoathiriwa kwenda kuendelea na masomo katika Shule jirani zilizo katika maeneo salama.
Prof. Mkenda ametoa maagizo hayo katika ziara yake hiyo, huku akikabidhiVitabu na Madaftari kwa Wanafunzi waliokumbwa na mafuriko katika shule ya Msingi na Sekondari Muhoro huku akiwataka Wazazi na Walezi kuzingatia agizo hilo.
Amesema, lengo la Serikali ni kuhakikisha Wanafunzi waliokuwa kwenye maeneo ya mafuriko wanaendelea na masomo wakati taratibu nyingine zikiendelea na kuwaelekeza Walimu kuwapokea Wanafunzi waliotoka maeneo ya mafuriko bila masharti na kutoa taarifa kwa Maafisa elimu, ili kupata idadi kamili ya waliorudi shuleni.
“Mwanafunzi akija kwenye shule yako mpokee mengine yatatatuliwa baadae haya ni maelekezo walimu wote wayasikie, Rais Samia Suluhu Hassan ameagiza tuongezee nguvu kuhakikisha wanafunzi kwenye maeneo yaliyoathiriwa wanaendelea na masomo,” amesema Prof. Mkenda.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Pro. Carolyne Nombo amesema Wizara hiyo itahakikisha wanafunzi wote walioathiriwa na mafuriko wanaendelea na masomo bila kikwazo, huku Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge akisema watazungumza na Wananchi ili wahamie maeneo salama.
Naye Afisa elimu Mkoa wa Pwani, Sara Mlaki ameeleza kuwa katika Wilaya ya Rufiji jumla ya Wanafunzi 7,264 wameathiriwa na mafuriko, huku Wilaya ya Kibiti Wanafunzi 824 wakikumbwa na adha hiyo.