Johansen Buberwa – Kagera.
Mamlaka ya mapato Tanzania – TRA, Mkoa wa Kagera imewataka wa wamiliki wa vyombo vya moto zikiwemo pikipiki za magurudumu mawili na matatu kulipa kodi kwa wakati ili kuichangia serikali mapato.
Hayo yamebainishwa mbele ya Waandishi wa Habari hii leo April 25, 2024 kwenye kikao maalum kati ya wadau wa Habari na Mamlaka hiyo, Afisa elimu kwa umma TRA mkoa wa Kagera, Rwekaza Rwegoshora.
Amesema, katika bajeti ya mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali imeweka kiwango cha kodi mpya kwa wamiliki wa pikipiki za biashara ambapo kwa mwaka mzima wanatakiwa kulipa kiasi cha shilingi 65,000 kwa mwaka, ambayo mmiliki wa anaweza kuilipiwa kwa awamu nne.
Aidha katika hatua nyingine Rwekaza amesema Serikali imekuwa ikipoteza mapato na kupata hasara kutokana na baadhi ya watu ambao sio waaminifu kwa kutumia njia zisizo sahihi yakiwemo magendo.
Amawasihi Wafanyabiashara kupitia milango ya forodha inayotambuliwa na serikali huku akiwaomba wananchi ndani ya Mkoa huo waendelea kutoa ushirikiano kwa mamlaka hiyo kwa kutoa taarifa pindi wanapoona viashiria vyovyote vya magendo.
Kwa upande wake meneja wa TRA Mkoa wa Kagera, Castro John amewashukuru waandishi wa habari kwa kuwa kiungo muhimu cha kuunganisha Mamlaka hiyo na Wafanyabiashara kwa kuhamasika kulipa kodi mkoani humo huku akisisitiza wafanyabiashara kuwa na matumizi sahihi ya mashine za EFD.