Kiungo wa Young Africans, Stephane Aziz Ki, amesema malengo yake ya kwanza msimu huu ni kuona anaisidia timu yake kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Aziz Ki ambaye ndiye kinara wa mabao katika ligi hiyo msimu huu akifunga mabao 15, amesema baada ya lengo la kwanza kutimia, ndipo atafikiria Tuzo ya Ufungaji Bora.
“Lengo langu kuu msimu huu ni kubeba ubingwa na sio kutwaa kiatu cha ufungaji bora, mpango wa ufungaji bora utakuja baada ya kushinda ubingwa,” amesema Aziz Ki.
Aziz Ki ambaye huu ni msimu wa pili akitumikia Young Africans, amehusika katika jumla ya mabao 22 kati ya 54 yalifungwa klabuni hapo msimu huu katika ligi, amefunga 15 na pasi za mwisho saba.
Akizungumzia kuhusu mkataba wake na Young Africans, nyota huyo amesema hayo ni mambo yake na waajiri wake ingawa alikiri kuwa anamaliza mkataba wa awali mwezi Juni, mwaka huu.
“Mkataba ni katı yangu na waajiri wangu sidhani kama ni sahihi kuweka hadharani, hivyo naamini nitamalizana vizuri na uongozi wangu,” amesema.
Nyota huyo raia wa Burkina Faso, amewataka mashabiki wa Young Africans kuendelea kuwa na imani na timu hiyo na kuwasapoti wanapokuwa wanacheza.
Katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Young Africans ipo kileleni kwa alama 62, ikifuatiwa na Azam FC alama 54 wakati Simba SC ikishikilia nafasi ya tatu kwa alama 46.