Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo – CHADEMA, Tundu Lissu amesema watu hutofautiana katika mambo mbalimbali ikiwemo itikadi za vyama na hata mambo yenye kuleta maendeleo kwa jamii na kwamba kuwa mpinzani sio kosa la jinai.

Lissu aliyasema hayo katika moja ya mahojiano maalum ambayo aliyafanya na Dar24 Media nyumbani kwake jijini Dar es Salaam na kudai kuwa viongozi wengi wa CHADEMA wamekuwa wakikamatwa kwa kubambikiwa makosa ambayo siyo ya kweli kutokana na tofauti zao.

Amesema, “Tulimwambia Rais Samia kukutana kwetu hakuna maana kama watu wetu, Viongozi wetu wanaendelea kushikiliwa na vyombo vya jinai kwa makosa ambayo siyo ya kweli, na hata yeye tulimwambia kwamba anajua makosa ni ya kubambikiwa si ya kweli, ujue kuwa mpinzani sio kosa la jinai.”

Aidha Lissu ameongeza kuwa, wakati alipokutana na Rais Samia Brussels nchini Ubelgiji Februari 17, 2022 alimuambia kuwa wao na Dunia hawamuelewi na hawatamuelewa iwapo anahubiri upendo kipindi ambacho Mwenyekiti wa upinzani yupo Gerezani kwa kesi ya ugaidi wa uongo, na Rais Samia aliahidi kuwaachilia huru.

Hata hivyo, chama hicho kimekuwa kikiendelea na maandamano na kufanya mikutano ya hadhara, wakihimiza Wananchi kupambania suala la Katiba mpya bila kuchoka wakiamini ndiyo suluhu ya kuliongoza taifa katika misingi ya haki, sheria na utawala bora.

EWURA yatangaza bei mpya za Mafuta, Petroli yapanda
Ajali ya kushangaza yajeruhi, yaleta uharibifu