Scolastica Msewa, Kibiti.

Mkuu wa mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge amesema Serikali inafahamu kazi kubwa inayofanywa na Wafanyakazi wa sekta, idara na Taasisi mbalimbali katika kumsaidia Rais kuwahudumia Wananchi.

Kunenge ameyasema hayo wakati akihutubia Katika kilele cha maadhimisho ya siku ya Wafanyakazi duniani kimkoa yaliyofanyika katika Wilaya ya Kibiti Mkoani Pwani.

Amesema, “Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ni Mfanyakazi Bora mchapakazi wa kwanza katika mkoa wa Pwani, anaboresha maslahi na miundombinu ya Wafanyakazi wa mkoa huu, anaboresha mazingira ya kazi na mazingira ya shule, sekta ya afya na tayari ameahidi kuboresha makazi ya Wafanyakazi katika sekta ya elimu na afya.”

Akizungumzia changamoto mbalimbali walizoziwasilisha kupitia risala ya Wafanyakazi, Mkuu huyo wa mkoa wa Pwani alisema tayari serikali imeanza kushughulikia ikiwa ni pamoja na suala la kikokotoo cha wastaafu.

Awali, Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania TUCTA mkoa wa Pwani, Kinyogoli Ramadhani aliomba Serikali kusaidia usafiri wa uhakika kwa Walimu wanaofundisha katika Shule za maeneo ya Kata za Delta ambao hutumia mitumbwi kufika eneo moja hadi jingine.

Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Mei 2, 2024
Hatujashindwa kusimamia usafirishaji - Mrisho