Licha ya mvua kubwa zilizosababisha mafuriko katika Wilaya ya Rufiji Mkoani Pwani, Shirika la umeme Nchini – TANESCO, limesema ubadilishaji wa nguzo za miti na kuweka za zege umesaidia kuzuia uharibifu ukilinganisha na mwaka 2020 ambapo nguzo 60 zilikatika na Wananchi kukosa huduma ya Umeme.
Akizungumza na Waandishi wa Habari ofisini kwake, Meneja wa TANESCO Wilaya ya Rufiji, Said Masoud amesema pia hali hiyo imesaidia kukabiliana na athari za kimazingira, ikiwemo mafuriko na hali hiyo inaashiria nia njema ya serikali ya kumtoa Mwananchi gizani kuwa sasa inakwenda kutimia.
Amesema, katika Wilaya za Kibiti na Rufiji kabla ya mvua walifanya matengenezo makubwa ikiwemo kubadilika nguzo za miti na kuweka nguzo za zege sehemu kubwa hasa katika eneo ambalo maji ya mto Rufiji yanakatisha.
Ameyataja maeneo hayo kuwa ni pamoja na Barabara ya kwenda Mloka Kipo, Ngalambe, Mbambe, Mpima, na maeneo yote yaliyokuwa ni mkondo wa maji yameimarishwa kwa kumewekwa nguzo za Zege.