Klabu ya Chelsea inahusishwa na mpango wa kutaka kumsajili eliyewahi kuwa Mlinda Lango wa Arsenal Wojciech Tomasz Szczęsny, itakapofika mwishoni mwa msimu huu.
Chelsea wanatajwa kuwa kwenye mpango huo, wakiamini Szczesny, anatosha kuwa sehemu ya kikosi ambacho kitaleta mapinduzi msimu ujao wa Ligi Kuu ya England.
The Blues inadaiwa kutovutiwa na uwezo wa Walinda Lango wake wa sasa Robert Sanchez na Djordje Petrovic huku Kepa aliopo Real Madrid kwa mkopo, naye anaonekana hatoshi klabuni hapo.
Hata hivyo inadaiwa kuwa Klabu ya Juventus inayommiliki Mlinda Lango huyo kwa sasa, ipo tayari kumuachia mwishoni mwa msimu huu, ikiwa ni mpango wa kutaka kuboresha kikosi chao kwa kuleta changamoto mpya kikosini.
Szczesny ambaye ni Mlinda Lango kutoka nchini Poland hakuwa na kipindi kizuri zaidi alipokuwa akiitumikia Arsenal.
Arsenal ilikubali kumuachia Szczesny mwaka 2017 baada ya kudumu klabuni hapo kwa miaka minane, akicheza michezo 132.
Akiwa Juventus kuanzia mwaka 2017 amecheza michezo 197, akitwaa mataji Ligi Kuu ya Italia ‘Serie A’ mara tatu msimu wa 2017–18, 2018–19 na 2019–20.
Kombe la Italia ‘Coppa Italia’ mara mbili msimu wa 2017–18 na 2020–21 na Supercoppa Italiana mara mbili mwaka 2018 na 2020.