Jina la Kocha Mkuu wa Klabu ya Brighton & Hove Albion Roberto De Zerbi limeibuka katika kinyang’anyiro cha kuwania nafasi ya Kocha Mkuu wa Mabingwa wa zamani wa Ujerumani FC Bayern Munich.
Uongozi wa FC Bayern Munich kwa sasa upo katika heka heka za kusaka Kocha Mkuu mpya wa kikosi chao, baada ya kufikia makubaliano ya kusitisha mkataba na kocha wao wa sasa Thomas Tuchel atakayeondoka mwishoni mwa msimu huu.
De Zerbi ambaye alikuwa hatajwi katika kinyang’anyiro hicho, jina lake limeibuliwa na Gazeti la Daily Mail mapema leo Ijumaa (Aprili 03), ikielezwa anajipanga kuondoka Brighton mwishoni mwa msimu huu, ili kufanikisha mpango wa kuelekea mjini Munich, Ujerumani.
Gazeti la Daily Mail limeripoti kuwa, Kocha huyo kutoka nchini Italia amedokeza kwamba anaweza kuondoka katika klabu hiyo wakati wa majira ya joto.
Gazeti hilo limeandika: “Meneja wa Ligi ya England ameibuka kuwa meneja anayepewa nafasi kubwa ya kukinoa kikosi cha FC Bayern Munich msimu ujao.
“De Zerbi aliibua wasiwasi juu ya mustakabali wake mwanzoni mwa msimu huu 2023/24, na kukataa kujitoa kwa ‘Seagulls’ huku akikiri alihitaji kuhakikisha anakuwa na ‘maono’ sawa na klabu.
Kabla ya kuhusishwa na The Bavarians, Kocha huyo aliwahi kuhusishwa na mpango wa kuhamia Liverpool na FC Barcelona, lakini klabu hizo zinaonekana kusitisha mpango huo, huku Arne Slot akikaribia kuteuliwa kuwa Kocha Mkuu wa The Reds na Xavi akiamua kusalia Camp Nou.
“De Zerbi mwenye umri wa miaka 44, anaweza kuondoka wakati wa majira ya joto, akiwa na fursa ya kuchukua jukumu la kukinoa kikosi cha moja ya klabu kubwa barani Ulaya.”