Baada ya kuondoka kwa Abdelhak Benchikha, Uongozi wa Simba SC kwa haraka umeanza mchakato wa kutafuta Kocha Mkuu mpya atakayerithi mikoba ya Mualgeria huyo ukipanga kukamilisha ishu hiyo kabla ya msimu huu kumalizika Mei 28, 2024.

Mabosi wa Simba SC walikaa kikao baada ya kuondoka kwa Benchikha aliyesepa na wasaidizi wake Farid Zemit na Kamal Bougnan, na kuamua kuanza mara moja mchakato wa kupata mrithi wake ambaye atakinoa kikosi cha klabu hiyo walau katika michezo mitatu ya mwisho msimu huu, ili ajue wapi pa kuanzia katika usajili wa dirisha kubwa likifunguliwa baada ya kumalizika kwa msimu.

Licha ya Simba SC kufanya kuwa siri, lakini taarifa zinabainisha kuwa Wekundu wa Msimbazi wanatafuta kocha haraka ili aweze kusimamia shoo nzima ya usajili ambao klabu hiyo imepanga kufanya kufuru kwa kushusha majembe yatakayoipambania na kurejesha ufalme ilioupoteza misimu mitatu sasa.

“Kama tulivyoongea mwanzo wachezaji wengi wanamaliza mikataba na tulisitisha mazungumzo ya kuwapa mikataba mipya. Sasa hatuna kocha mkuu nani atasajili? Tunataka kupata kocha kabla ya ligi kuisha ili awaone wachezaji na kujua anaanzia wapi kwenye usajili. Pia kushauri nani atoke na nani abaki kati ya hawa ambao mikataba yao inafika ukomo mwishoni mwa msimu huu,” amesema mmoja wa viongozi wa Simba na kuongeza:

“Hatutatangaza makocha waombe kazi kwetu, lakini tuna baadhi ya makocha Tuliwaona na tumeanza maongezi. Tunataka kufanya jambo hili kwa weledi zaidi na kupata kocha atakayeendana na falsafa zetu na kutupa kile tunachohitaji.”

Licha ya kutoweka majina ya makocha wanaozungumza nao, lakini moja ya sifa za kocha ambaye Simba SC inamtaka kwa sasa ni yule atakayekuwa na ubora wa kutengeneza wachezaji na kuleta usawa kikosini.

Simba SC inataka kocha atakayewajengea uwezo wachezaji na kupata timu itakayocheza kwa muunganiko, umoja na mshikamano bila kuwa na matabaka.

Sifa nyingine ambayo Simba SC inaizingatia kupata kocha mpya ni lazima awe na uzoefu wa kutosha kwenye soka la Afrika, hususan katika michuano ya CAF ambayo timu hiyo kwa miaka ya hivi karibuni imekuwa ikiishia robo fainali.

Imebainika kuwa katika makocha wanaofuatiliwa kwa karibu na vigogo wa Msimbazi wengi wao waliwahi kuzungumza nao hapo kabla, lakini madili yao ya kutua unyamani hayakukamilika kwa sababu mbalimbali.

Miongoni mwa makocha hao ni Msenegali Lamine N’Diaye ambaye kwa sasa ni kocha wa TP Mazembe, lakini kabla ya hapo aliwahi kuzinoa Horoya ya Guinea, Al Hilal ya Sudan, Maghreb de Fes ya Morocco, Coton Sports ya Cameroon na timu ya taifa ya Senegal.

Kocha huyo msimu huu ameifikisha TP Mazembe hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ukiwa ni msimu wake wa kwanza.

Mwingine ni Mreno Alexandre Santos, kocha mkuu wa Petro de Luanda ya Angola ambayo msimu huu imetolewa katika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Kocha huyo pia aliwahi kuwindwa na Simba SC 2022, lakini dili lake halikukamilika.

Yupo pia Omar Najhi, Mwingereza mwenye asili ya Morocco ambaye alizidiwa kete na Benchikha kwani alikuwa kwenye rada za Simba wakati alipofukuzwa Oliveira Roberto ‘Robertinho’. Kocha huyo aliyewahi kuzifundisha Wydad Casablanca na Mouloudia za Morocco kwa sasa yupo huru baada ya kuchana na Ittihad Tanger ya nchini humo.

Hao ni baadhi ya makocha ambao inaelezwa wapo kwenye listi ndefu iliyopo mezani kwa Simba huku Juma Mgunda naye akifikiriwa kubakizwa kikosini hapo kama kocha msaidizi endapo watapata kocha mkuu.

Kwa sasa Simba SC ipo chini ya Mgunda anayekaimu nafasi ya Kocha Mkuu akisaidiwa na Selemani Matola aliyewahi kuwa kiungo na nahodha wa zamani wa timu hiyo.

Simba SC iliyo nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi na alama 47 baada ya mechi 22, bado inaendelea kupambana katika mawindo ya alama tatu za michezo iliyosalia msimu huu 2023/24.

CHADEMA kwafukuta: Lissu adai rushwa imekithiri ndani ya chama
Hali ya Vyombo vya Habari kimaudhui si nzuri